HATIMAYE, Mwangalizi Mkuu wa Kanisa la Scoan (Synagogue Church of All
Nations), Mtume na Nabii Temitope Balogun Joshua ‘TB Joshua’ ametua
Bongo juzi akitokea nchini Nigeria, maalum kumshuhudia Rais Mteule wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’
akiapishwa leo.
TB Joshua aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) na kupokelewa na JPM akiwa ameongozana na mkewe, mama
Janeth Magufuli na wasaidizi wengine wa JPM.
Kwa mujibu wa Wabongo waliobahatika kusalimiana na TB Joshua kwa
kushikana mikono, ujio wa nabii huyo umeonesha alivyoshindwa kulala
nchini mwake wakati Magufuli akiapishwa jijini Dar, ikizingatiwa kuwa,
alimtabiria kushinda nafasi hiyo ya urais.
“Jamani, naye (TB Joshua) kajisikia raha Magufuli kushinda. Mtu
aliyemtaribiria kuwa rais, kashindwa kulala nchini mwake, akaona aje
aone kama ni kweli,” alisema mfanyakazi mmoja wa uwanja huo wa ndege.
Mara baada ya kutua uwanjani hapo, TB Joshua alikwenda Ikulu ya
Magogoni, Dar kwa ajili ya kumsalimia rais anayemaliza muda wake leo,
Dk. Jakaya Kikwete ‘JK’, pia kumpongeza kwa kufanikisha uchaguzi mkuu
kwa uhuru na amani.
Kwa mujibu wa itifaki, mteule huyo na aliyekuwa mgombea mwenza, Samia
Suluhu Hassan wataingia uwanjani hapo kabla ya JK, lakini mara baada ya
kuapishwa, Dk. Magufuli atakuwa wa kwanza kutoka akiwa katika msafara
wenye ulinzi mkali kuelekea ikulu kwa maisha rasmi ya urais.
Aidha, Dk. Magufuli atafuatiwa na makamu wake kabla ya viongozi wengine wakiwemo marais wastaafu.
Tukio kama hilo liliwahi kufanyika mwaka 2005 wakati JK alipoapishwa
kuchukua nafasi ya rais aliyemaliza muda wake, Benjamin William Mkapa.

Note: Only a member of this blog may post a comment.