Wednesday, November 11, 2015

Anonymous

Tathmini ya CCM Yaonesha Edward LOWASSA Kuwa Mwiba Mchungu Kwao

Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro (UVCCM), Yasini Lema, ‘amefunguka’ kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita namna ulivyokiathiri chama hicho na kukifanya kipoteze majimbo ya uchaguzi ya Siha, Same Mashariki na Moshi Vijjini waliyokuwa wakiyashikilia kwa zaidi ya miaka 15.

Lema amedai kuangushwa kwa mawaziri wawili wa serikali iliyopita, Aggrey Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Anne Kilango Malecela (Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk. Cyril Chami, kulitokana na ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Lema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Nipashe, kuhusiana na tathimini yao waliyoifanya Novemba 7, mwaka huu baada ya kupitia zoezi zima la uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema Lowassa ndiye aliyeisaidia Chadema kuwapokonya majimbo hayo kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi wakiwamo pia baadhi ya makada wa CCM ambao hawakufurahishwa na kitendo cha Kamati Kuu ya chama hicho kuliengua jina lake wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho.

“Chadema imefanikiwa kuchukua majimbo ya CCM kutokana na mkakati wa Lowassa pamoja na kuhama kwake, kitu ambacho kilitengeneza mpasuko ulioiua CCM na wagombea wake,” alisema.

Alidai kulitokea usaliti ndani ya CCM kwa madai kulikuwa na kundi ambalo lilikuwa likiendelea kushiriki vikao vya ndani huku likikerwa na kuondoka kwa Lowassa jambo ambalo lilisababisha chama hicho kushindwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Aidha, akizungumzia mkakati wa CCM kuyarejesha mikononi mwake majimbo ya Moshi Mjini na Rombo, Lema alidai kuwa sababu ya kushindwa kwao ni kutokana na wagombea wa nafasi za ubunge kupitia chama hicho kupora mamlaka ya viongozi wa wilaya.

“Wagombea ubunge katika majimbo haya mawili walikuwa na nguvu zaidi katika chama, atakalolisema yeye na atakalopanga ndilo atakalolisimamia lifanyike. Ukweli ni kwamba viongozi wa wilaya nao waliwaogopa, huku kampeni zao zikikwepa kabisa kuwashirikisha viongozi wa chama ngazi za matawi na kata” alisema Lema.

Alisema pamoja na kwamba CCM kilianzisha vikosi kazi maalum kwa ajili ya kutafuta kura, lakini katika hali ya kushangaza wagombea wao wa ubunge katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Kilimanjaro, walijiweka kando kuwatumia viongozi wa matawi na ngazi ya kata.

Sababu nyingine ya kupoteza viti vingi vya udiwani alisema ni wagombea wao kujiaminisha kwamba CCM ingewaletea fedha nyingi kwa ajili ya kampeni huku wengine wakiamini wangesaidiwa na wagombea ubunge ambao waliamini walikuwa na fedha nyingi kuwashinda wagombea wa vyama vya upinzani.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.