Rais
John Magufuli amemtumia salamu za pole Rais wa Ufaransa François
Hollande, kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyogharimu vifo vya
watu 127.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Rais Magufuli alisema Serikali yake inaungana na wapenda
amani wote duniani kulaani tukio hilo lililogharimu maisha ya watu
wengi.
Awali
taarifa za AFP zilisema serikali ya Ufaransa iko kwenye hali ya
tahadhari baada ya kutokea mashambulizi mfululizo ya kutisha kufanywa
kwenye maeneo maarufu jijini Paris Ijumaa usiku na kusababisha vifo vya
watu zaidi ya 127.
Tayari kikundi cha wanamgambo wa ISIS kimeshasema kimehusika na mashambulizi hayo.
Waliofanya
mashambulizi hayo walilenga maeneo mepesi kufikika ambako watu walikuwa
wakiendelea kusherehekea wikiendi kwenye eneo ambalo hufanyika
matamasha ya sanaa, mahoteli na baa, na kwenye Uwanja wa Taifa wa
Ufaransa ambako mechi ya kimataifa ya soka ilikuwa ikichezwa.
Ikiwa imeshatingishwa na shambulizi la kigaidi la Januari, jiji la Paris lilikumbwa na kiwewe na hali ya kuchanganyikiwa.
“Ni
kama Paris imetekwa kwa sasa,” alisema mwandishi wa habari wa kituo cha
televisheni cha CNN, Anne-Charlotte Hinet baada ya watu hao kushambulia
maeneo sita kwenye jiji la Paris.
Mamlaka ziliwataka wananchi kutotoka nje, huku Jiji likiwa limefunga majengo mengi ya umma na kuongeza ulinzi wa kijeshi.
Mashuhuda
walisema kwenye eneo linachukua zaidi ya watu 1,500 ambako tamasha la
muziki lilikuwa linafanyika, walieleza jinsi washambuliaji hao
walivyokuwa wakifyatua risasi kuelekea kwa watu.
Mlipuko
uliotokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France, ambao
umeelezewa kuwa ulikuwa wa kujitoa muhanga, ulikuwa wakati timu za taifa
za Ujerumani na Ufaransa zikicheza, na kusababisha Rais Francois
Hollande kuondolewa uwanjani.
Note: Only a member of this blog may post a comment.