RAIS
mpya wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameambiwa kama ni kweli amenuia
kukomesha biashara ya madawa ya kulevya nchini, basi awashughulikie
wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza bidhaa hiyo.
Anaweza
kuanza kwa kuifanyia kazi orodha ya wafanyabiashara 104 magwiji wa
madawa hayo, orodha ambayo alipewa mtangulizi wake, rais mstaafu Jakaya
Kikwete alipoingia madarakani Desemba 2005.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya madhehebu
ya dini nchini, Askofu William Mwamalanga amesema orodha hiyo
iliguswaguswa tu na uongozi uliopita.
“Sisi
viongozi maaskofu na masheikh 120 tuliokutana kwa siku tatu mjini
Arusha kwa lengo la kutathmini athari za tatizo la matumizi ya
mihadarati kwenye Nchi za Maziwa Makuu, tunampongeza Rais John Magufuli
kwa kuweka wazi ajenda ya kupambana na janga hili nchini. Tunamhimiza
aishughulikie ile orodha tuliyomkabidhi mtangulizi wake,” amesema Askofu Mwamalanga.
Hayo
yamo katika tamko la kongamano lililoshirikisha viongozi wa dini wa
nchi za kanda ya Maziwa Makuu kwa ushirikiano wa mashirika ya kidini ya
Ujerumani, Marekani na Afrika yanayopambana na biashara ya usafirishaji,
usambazaji, utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana katika nchi za
Ulaya na kanda hii ya Kusini mwa Afrika.
“Tunaungana
naye katika kusimamia ajenda aliyoitangaza katika hotuba yake ya
uzinduzi wa Bunge la 11; tunadhani wakati umefika awezeshwe kutungwa
sheria ya adhabu ya kifo ya kuwashughulikia wafanyabiashara wakubwa wa
‘unga’ kama ilivyo nchini China. Atakuwa ametoa mchango muhimu katika
kupunguza uharibifu unaofanywa dhidi ya maelfu kwa maelfu ya vijana wa
Afrika, wakiwemo Watanzania."
Askofu
Mwamalanga wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste ameonya Tanzania ni
muathirika mkubwa wa tatizo hilo kwa miaka mingi sasa kama ilivyo kwa
janga la rushwa na ufisadi, na kusisitiza panahitajika sheria hiyo
ishikiliwe kwa uimara.
Amesema
hotuba za maneno matupu haziwezi kutokomeza rushwa na biashara ya
mihadarati kwani wamiliki wakubwa ni watu wenye utajiri mkubwa kwa hivyo
moyo alioonesha rais mpya utakuwa ukombozi.
Mwanzoni
mwa mwaka 2006, Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii
ya madhehebu ya dini nchini ilikutana na Kikwete na kumkabidhi orodha ya
magwiji 104 wa mihadarati “kiukweli hapajawa na mafanikio kwani leo miji yote Tanzania vijana wanafanyabiashara hiyo kama njugu.”
Askofu
Stave Marks na Profesa George Furhaman kutoka Ujerumani wametambua
mchango wa Kamati ya Askofu Mwamalanga wa kukabidhi orodha ya magwiji wa
mihadarati kwani Tanzania haipaswi kutumiwa kama uchochoro wa kupitisha
bidhaa hiyo kwa asilimia 11 kwenda nchi za Kusini mwa Afrika na Ulaya.
Orodha
hiyo inajumuisha majina ya watu waliokuwa wakitumia mgongo wa vyeo na
nafasi zao serikalini na pia ukaribu wao na viongozi wakuu na marais wa
mataifa mbalimbali ya Afrika Tanzania wakiwemo maaskofu, wachungaji,
manabii na masheikh wa uongo.
Mbele
ya kongamano hilo, Padre kutoka Zambia alikiri kuwahi kuwa kinara wa
mtandao mahsusi wa kusafirisha madawa ya kulevya kupitia Dar es Salaam,
Tunduma, Lusaka na kuingia Afrika Kusini kati ya mwaka 2005 na 2007.
Alidai
kuiacha kazi hiyo baada ya kubaini kuwa jina lake lilikuwemo kwenye
orodha aliyokabidhiwa Kikwete mwaka 2006 na amesema walioamua kuacha
kama yeye ni “mashujaa kwani wengi wao wameishia kunyongwa nchini China.”
Masheikh
Abdallah Zuberi wa Mombasa na Kassimu Mohmed wa kisiwani Pemba ameitaja
Zanzibar kama kitovu kikubwa cha mihadarati kwenye ukanda huu kutokana
na usimamizi dhaifu wa sheria.
Sheikh
Mohamed amesema kama jitihada za kudhibiti viongozi wakubwa
wanaoendeleza biashara hiyo zitaachwa kwenye ahadi za wanasiasa walioko
madarakani, ipo hatari kwa nchi nyingi za Afrika kuongozwa na magwiji wa
‘unga’ hasa kwa kuwa safari hii wapo baadhi yao wameshinda uchaguzi
mkuu na kuingia bungeni.
Amewataja
watu wanane alioita mapapa wa biashara hiyo wanaoishi Dar es Salaam,
Arusha na Zanzibar, aliosema wamewatia mfukoni viongozi wakubwa
waliochaguliwa ndipo serikali ikabaki kuhimiza tu katika danganya toto
huku ikiichezea orodha.
Note: Only a member of this blog may post a comment.