Sunday, November 15, 2015

Anonymous

AL- SHABAB WASHAMBULIA BUNGE LA SOMALIA!


ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Mpenzi mfuatiliaji wangu, wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo mapambano kati ya Al-Shabaab na majeshi ya Serikali ya Somalia yakisaidiwa na yale ya kigeni yalivyokuwa yakipambana. Licha ya vipigo vikali kutoka kwa majeshi ya Afrika, wapiganaji hao walishambulia Kambi ya Wakimbizi ya Daadab iliyopo kwenye mpaka wa Somalia na Kenya ambayo inahesabiwa kuwa moja ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. SASA ENDELEA…

Tayari Somalia imeshuhudia mashambulizi ya kigaidi ya Al-Shabaab kwenye miji na maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo. Pia imeshuhudia mauaji ya watu wengi wasiokuwa na hatia.

Katika hali kama hiyo, ilibidi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kuingilia kati na kueleza kuchukizwa na shambulizi lingine baya lililofanywa na Wanamgambo wa Al-Shabaab la uvamizi wa Bunge la Somalia ambapo watu zaidi ya kumi waliuawa.

Duru za kiusalama nchini humo zilieleza kwamba shambulio hilo lililohusisha mashambulizi ya mabomu na watu wenye silaha wakiwa wamevaa milipuko, hatimaye lilifikishwa mwisho baada ya zaidi ya saa nne za mapambano na Majeshi ya Somalia na lile la mataifa ya Afrika la kulinda amani (AMISOM).

Ripoti ya tukio hilo ilieleza kwamba, wajumbe 15 wa baraza hilo la usalama walilalama juu ya tukio hilo.
Wajumbe hao walichukizwa mno na kitendo cha Al-Shabaab kushambulia bunge, taasisi ambayo inawakilisha watu wa Somalia na matumaini yao halali ya amani, usitawi na uthabiti.

Shambulio hilo la kihistoria lilisababisha umwagikaji wa damu nyingi na matukio mengine ya kiwendawazimu ya kigaidi ambayo hayakupaswa kupuuzwa hata kidogo.

Matukio hayo yasiyokuwa ya kibinadamu yalikemewa na kupingwa vikali na majeshi ya kulinda amani ya kimataifa ya Afrika pamoja na wahusika wengine waliopigania amani nchini Somalia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon alilishutumu vikali shambulio hilo akieleza namna ambavyo wabunge walihitaji mshikamano na uungwaji mkono katika kukabiliana na matukio kama hayo kwenye chombo kikubwa cha serikali kama bunge.
Alikaririwa: “Hakuna uhalali wowote kwa shambulio kama hilo.”
Hata hivyo, hakuna idadi kamili ya watu waliouawa iliyotolewa mara moja lakini maafisa wa polisi na duru za serikali nchini humo zilieleza kuwa zaidi ya watu 10, ikiwa ni pamoja na washambuliaji kadhaa walipoteza maisha.
Baadaye vyombo vya habari vya ndani nchini humo vilieleza kuwa watu zaidi ya 20 huenda walipoteza maisha, ikiwa ni pamoja na washambuliaji nane.

Msemaji wa Al-Shabaab alithibitisha kuwa kundi hilo lilihusika kikamilifu na shambulio hilo.
Ni katika tukio hilo ambapo Waziri wa Somalia aliyehusika na usalama, Abdikarim Hussein Gulled alitangaza kujiuzulu baada ya shambulizi hilo la kundi lenye msimamo mkali wa Kiislam katika jengo la bunge la nchi hiyo.

Gulled alitoa tangazo hilo katika redio ya taifa mjini Mogadishu, ikielezwa kwamba alikuwa katika mbinyo kutoka kwa bunge kuhusiana na hali iliyokuwa ikiendelea ya kutokuwa na usalama katika taifa hilo.
Wakosoaji wa mambo ya kiusalama walidai kwamba Gulled alikosa uzoefu katika nyanja hiyo ya usalama katika kipindi kibaya cha mashambulizi ya Al-Shabaab.

Ilibidi Rais Hassan Sheikh Mohamud afupishe ziara yake nchini Afrika Kusini akisema aliamua kurejea nyumbani kutokana na hali tete ya nchi hiyo.
Mbali na mauaji, zaidi ya watu 30 walijeruhiwa vibaya ikiwa ni pamoja na wanajeshi 14 wa Jeshi la Somalia na watano wa Jeshi la Afrika la kulinda amani.

Serikali ya Somalia imekuwa ikipambana na Kundi la Al-Shabaab kwa miaka kadha sasa kwa msaada wa jeshi la mataifa ya Umoja wa Afrika.
Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.