“Jamani muwe makini na antena zenu za tv wakati wa kuzirekebisha, hasa kwa wale ambao hawana utaalam na vitu vya umeme.”
Hiyo ni kauli ya Abrahaman Juma, mkazi
wa Mtoni Kwaazizi Ally, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam aliyepata
ajali ya kuunguzwa na umeme wakati akirekebisha antena ya tv yake.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 30
anasema amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu 0ktoba 28,
mwaka huu baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Temeke, Dar ambapo
wataalam wa huko walimwambia kuwa anastahili kwenda Muhimbili kwa hatua
zaidi za kitabibu.
Akisimulia mkasa huo Juma anasema:
“Nilifika hapa Muhimbili Oktoba 28, mwaka huu, nikiwa sijakatwa mikono lakini ilikuwa nyang’anyang’a kwa kuunguzwa na umeme.
“Tatizo kubwa ilikuwa umeme ambao uliniathiri mikono yangu wakati narekebisha antena ya tv yangu ili iweze kuonesha vizuri.
“Tv yangu ilikuwa ikionesha chenga sana
hivyo nikaamua kupanda juu ya nyumba ili kurekebisha bomba lililokuwa
na waya wa tiv hiyo.
“Nilifika juu nikawa nimeshika bomba
lenye antena nikawa nalizungusha huku nikiwauliza walio ndani kama picha
zinaonekana vizuri.
“Kwa mujibu wa aliyekuwa akiniongoza mle
ndani, alikuwa akisema ‘bado, bado’ nami nikawa naendelea kuhangaika
kuzungusha bamba, ghafla likagusa waya wa umeme ukaniunguza.
“Nilishitukia nikitupwa chini, nilipiga
kelele ndipo mke wangu alipomuacha mtoto wa miezi mitatu ndani na kutoka
nje mbio kwa lengo kuja kuniokoa, akanikuta nipo chini nikigaragara kwa
maumivu makali na mikono yangu ikiwa umeungua sana.
“Mke wangu aliomba msaada kwa watu ili niweze kukimbizwa hospitalini na nikawahishwa katika Hospitali ya Rufaa Temeke, Dar.
“Tulipofika huko nilijieleza na
madaktari wakatushauri kuwa nihamishiwe hapa Hospitali ya Taifa,
Muhimbili ili niweze kupatiwa matibabu zaidi.
KUKATWA MIKONO
“Nilipofikishwa hapa Muhimbili madaktari
wakasema umeme uliniathiri sehemu kubwa ya mikono yangu hivyo
isingeweza kuunga na dawa pekee ni kuikata. Ndiyo hivyo, nimekatwa
mikono.
MGUU NAO ULIDHURIKA
“Pia ule umeme ‘ulinipiga’ pia mguuni na kusababisha mguu huo kupata majeraha, nashukuru madaktari wamenitibu.
KUMBE ALIKUWA DEREVA
“Nasikitika kukatwa mikono kwa sababu
nilikuwa nimeajiriwa hivi karibuni katika Kampuni ya Mamba Auto Spere
kama dereva, nina mke na mtoto mmoja mwenye umri wa miezi mitatu, sasa
wataishije na mikono iliyokuwa ikinipa riziki sina?” alihoji huku
akitokwa machozi.
TAHADHARI
Watu wengi wamekuwa wakipigwa na shoti
ya umeme baada ya bomba ya antena kuangukia nyaya za umeme. Wapo
waliofariki dunia kutokana na madhara hayo. Ni vema kuhakikisha bomba la
antena linachimbiwa mbali na nyaya za umeme.
Watanzania Abrahaman amepata
kilema cha maisha kama umeguswa na habari yake wasiliana naye kwa simu
namba 0656 362172 ambayo kwa sasa anaishikilia mdogo wake au mtembelee
wodi namba 23 SEWA HAJI, Muhimbili- Mhariri.

Note: Only a member of this blog may post a comment.