Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Na Said AllyKOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametamka kuwa yupo katika mikakati ya kuhakikisha anawaongezea mbinu zaidi washambuliaji wa kikosi hicho, wakiwemo Amissi Tambwe na Donald Ngoma kutokana na kuona kuwa hawatumii vyema nafasi wanazozitengeneza licha ya kwamba wamekuwa wakifunga mabao.
Pluijm ameiongoza Yanga kuweza kukaa kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 19 ambapo katika michezo hiyo wachezaji wa timu hiyo wamefunga mabao 18 wakiwa ndiyo timu inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi wakiwazidi Azam mabao saba ambao wapo katika nafasi ya pili wakifunga mabao 11.
“Ni kweli tumekuwa tukishinda mabao mengi tu katika kila mchezo wetu lakini binafsi sifurahishwi na jinsi wachezaji wangu wanavyoshindwa kutumia vyema nafasi wanazozitengeneza ambazo huwa ni nyingi kuliko mabao ambayo tunashinda.
“Sijui ni kuridhika na mabao ambayo tunakuwa tunafunga lakini mimi kwa upande wangu naona linaweza kuwa tatizo siku moja kama tutacheza na timu ambayo itatufunga kisha wakazuia ushindi wao, tunaweza kujikuta tukipoteza mchezo huo.
“Lakini tayari nimeweza kulibaini tatizo hilo ambapo kwa sasa naenda kulifanyia kazi kwa kuwanoa zaidi washambuliaji wangu wawe makini katika kufunga kwenye kila nafasi tutakayoipata,”alisema Pluijm.
Note: Only a member of this blog may post a comment.