Wednesday, October 14, 2015

Anonymous

Mwili wa Dk. KIGODA Kuwasili Nchini Leo.

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, unatarajiwa kuwasili leo kutoka nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu na maziko kufanyika kesho.

Mwakilishi wa familia, Athumani Mdoe, alisema mwili utawasili leo saa 9:00 alasiri katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupelekwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo kwa hifadhi.

Mdoe alisema mwili huo utaagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda mjini Handeni kwa maziko kesho.

Dk. Kigoda alifariki dunia juzi jioni katika Hospitali ya Apollo, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. Dk. Kigoda ambaye alikuwa Mbunge wa Handeni, alikuwa anatetea nafasi yake hiyo baada ya kuteuliwa na Chama chake Cha Mapinduzi (CCM).
 
Ni Waziri wa pili kufariki dunia katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri wa kwanza kufariki dunia katika kipindi hiki ni Celina Kombani, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Septemba 24 , mwaka huu.

Wagombea wengine wa ubunge waliofariki dunia kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi ni Mohamed Mtoi, Septemba 13, mwaka huu, ambaye alikuwa anagombea ubunge Jimbo la Lushoto kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Estomiah Millah, Oktoba 9, mwaka huu.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.