MPENZI
msomaji wa simulizi hii tamu ya Mrisho Mpoto, wiki iliyopita tuliishia
pale Mrisho alipoamua kuanzisha Kipindi cha Bongo Dar es Salaam na
kufanikiwa kumuweka Dude lakini Dude huyohuyo akalewa sifa na kutaka
kumgeuka ambapo alienda Televisheni ya Taifa (TBC) na kudai apewe
mkataba mpya bila Mrisho kujua. Alikataliwa, je unajua kilichoendelea?
Songa nayo sasa…
“TBC wakaendelea kumgomea Dude kwamba hawawezi kuukatisha mkataba kwa kuwa sikuwepo na wala sijakubaliana naye. Kwa ufupi tu ilikuwa ni stori ndefu sana.”
Bado umeniacha njia panda kaka, sijaelewa mwisho wa hili, ikawaje sasa?
“Tulikaa kidogo nikaona isiwe tabu, nikaamua kukatisha kabisa Bongo Dar es Salaam. Kwa kuwa nilikuwa nimesajili hivyo Dude alishindwa kusajili sehemu nyingine kwa kipindi hicho sababu nilikuwa tayari nimeshasajili hivyo alishindwa kutumia jina Bongo Dar es Salaam.
“Baada ya kukaa kipindi kirefu kidogo, alirudi na kuniomba bwana nimeenda EATV, Azam TV akaniomba sana tu. Nikaona kwa kuwa nimeshatoka na sikuwa nahitaji kuwa tena na Bongo Dar es Salaam kwa kipindi kile, nikaamua kumuachia.”
Baada ya hapo nini kiliendelea?
“Dude yupo anaendelea kuiweka sawa ataitoa tu. Lakini baada ya hapo ninachoweza kusema kuwa nilikuwa sina kinyongo chochote hivyo nilinunua Ballon (Toyota) nyingine ile ya kwanza nikamuachia Dude, nikajikita zaidi kwenye sanaa.
“Kweli tukaanzisha kampuni inaitwa Mpoto Arts Production. Nikawa na jina kubwa japokuwa sikuwa na ofisi maalum, nilikuwa nakodisha maeneo tofauti ya mazoezi lakini mwisho wa siku tukapata sehemu Kinondoni jijini Dar ambapo Tesha alichukua mkopo na kuingiza vyombo vya muziki na vifaa vya ofisi.”
Huyo Tesha alikuwa na asili ya Kihindi?
“Hapana ni Mchaga. Tukaenda kwa muda mrefu lakini mwisho wa siku tukapishana Kiswahili (kutokuelewana), ikabidi wanipeleke mahakamani.”
Ilikuwaje mkapishana Kiswahili, unaweza kufafanua kidogo?
“Ujue ilifika mahali, huyu Tesha alikuwa akileta ndugu zake na kuwaweka kwenye vitengo mbalimbali ndani ya ofisi. Walivyonishtaki kesi iliyumbayumba kwa muda wa mwaka mzima, nikaomba tuyamalize nje, basi tukakubaliana kugawana mali. Wao wakachukua fedha na baadhi ya vitu ikabidi nianzishe kampuni nyingine ndiyo hii ya Mpoto Gallery Theatre kwa hiyo katika ule mgawo mimi nikabakiwa na ofisi.
“Nikaanza ofisi nikiwa na mtu mmoja, nikaanza kutafuta mtu mmojammoja, kampuni ikaanza kuongezeka nikatafuta wasanii, wafanyakazi kama ishirini na nane.”
Mlikuwa mnafanya na shoo?
“Yeah tulikuwa tukipiga shoo kila wikiendi pale Mzalendo Pub (Kijitonyama), Masaki, kwenye baa mbalimbali, nikaanza kufanya matangazo ya kiserikali, jina likaongezeka mara mbili na tuzo zikamiminika zaidi.”
Hapohapo kwenye tuzo Mrisho, hadi sasa una tuzo ngapi ulizoshinda?
“Mpaka sasa nina tuzo tano.”
Mpaka hapa tulipofikia, ni tukio gani ambalo huwezi kulisahau maishani mwako, kabla hatujaendelea tafadhali?
“Huwa nakumbuka sana maneno ya marehemu mama yangu kabla ya kufariki dunia aliwaambia watu; ‘Naombeni mniitie Mrisho.’ Akaniambia; ‘Mwanangu mimi nilikuwa baba yako na nilikuwa mama yako, unahisi umekua?’ nikamwambia nimekua, akaniambia; ‘Mwanangu nakuomba sana, katika kukulea nataka uishi kwako, umeshajenga?’ nikamwambia; ‘Nimeshajenga na nataka siku moja uende ukaishi kwenye nyumba yangu.’ Akacheka sana na kuniambia…
Usikose wiki ijayo.
Note: Only a member of this blog may post a comment.