Mwandishi Wetu
MAPENZI yanatingisha
dunia! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia nyota wawili wa Bongo Fleva,
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kuzinguana
laivu nchini Marekani, Risasi Jumamosi limevujishiwa na lina mchapo kamili.
Chanzo makini kilichoshuhudia sakata
hilo lililotokea hivi karibuni nchini Marekani kulipokuwa na hafla ya
utoaji wa tuzo za Afrimma ambapo Diamond alitwaa 3 huku Dimpoz akipata
1, kimenyetisha kuwa, wawili hao walizinguana wakiwa wanataka kuingia
kwenye ukumbi ulioandaliwa kwa ajili ya utoaji wa tuzo hizo.
“Walipokuwa wanaingia ukumbini, Dimpoz
akakutana na Diamond sasa Diamond akataka kumsalimia ndipo Dimpoz
akachomoa na kumpa maneno ya kejeli ambayo yalimkasirisha nusu
wazichape.
“Kila mtu alijua jamaa watashikana
mashati. Lakini sema ile busara ya haraka iliwajia, hawakufikia hatua
hiyo mbaya,” kilisema chanzo.
CHANZO CHA BIFU
Kikaendelea: “Unajua Dimpoz alikataa
kupokea salamu ya Diamond maana anasema ni mnafiki. Anadai kwamba,
Diamond anapokuwa na watu anajifanya hana tatizo na Dimpoz lakini akiwa
na marafiki wa Dimpoz huwa anamzungumzia vibaya na wakikutana na Dimpoz
anamsalimia kinafiki ndiyo maana mwenzake akamaindi.”
WEMA ATAJWA
Kikizidi kulipambanua bifu la mafahari
hao wawili, chanzo hicho kilidai kuwa, sababu kubwa ya bifu hilo ilianza
muda mrefu baada ya Diamond kumhisi Dimpoz anatembea na Wema Sepetu
‘Madam’ ambaye alikuwa mpenzi wake kwa muda mrefu kisha akamwagwa.
“Kumbe Diamond ana kinyongo na mwenzake.
Alimwagwa na Wema lakini nafikiri bado moyoni anampenda sana. Sasa
alipoona siku chache baada ya kuachana, ghafla mrembo huyo akaonekana
katika pozi tata na Dimpoz, akamuwekea bifu pasipo hata kumuuliza kama
ni kweli au la,” kilisema chanzo na kuongeza:
“Tangu hapo, Diamond amekuwa akimsema
vibaya Dimpoz kupitia marafiki zake kitu ambacho Dimpoz anakiona ni
unafiki kwani hamwambii mwenyewe. Huwezi amini kule Marekani, Diamond
alikuwa ndiye aliyetangulia kufika lakini badala ampokee mwenzake ambaye
ni mgeni, akampotezea halafu ukumbini akajifanya anamsalimia.”
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ubuyu
kuwa, kitendo cha wawili hao kuzinguana ukumbini wakati wanatokea sehemu
moja kiliwashangaza Wabongo waishio nchini humo ambao walikwenda
kushuhudia utoaji wa tuzo hizo kwani walitegemea wawili hao wangekuwa
kitu kimoja.
“Wabongo wenzao waishio Marekani
waliwashangaa sana. Hawajui kwamba huku ndiyo walitakiwa kuonesha umoja
wao. Kwanza ndiyo wanainuka katika tuzo kubwa halafu wao wanaleta za
uswahilini, itawagharimu siku moja,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupenyezewa ubuyu huo,
mwanahabari wetu alianza kumtafuta Dimpoz ili aweze kutoa ufafanuzi juu
ya kile kilichotokea ambapo alipopatikana, alifunguka:
“Daah! Nani kawapa hizo habari? Nyinyi kweli mnajua kunusa. Ni kweli tulipishana na jamaa (Diamond) kule Marekani.
“Lakini si unajua tena… pengine Diamond
ana kinyongo chake na mimi sipendi mtu anayeishi kwa vinyongo, ndiyo
maana nilikataa salamu yake, yakatokea hayo lakini kimsingi namshukuru
Mungu hatukukunjana wala nini.”
DIAMOND SASA
Jitihada za kumpata Diamond ili aweze
kueleza kwa upande wake hazikuzaa matunda kufuatia kuwepo kwa taarifa
kuwa alikuwa safarini nje ya nchi.
“Jamaa siyo rahisi kumpata sababu yupo
safarini nje ya nchi labda umcheki tena baadaye,” alisema mtu wa karibu
na Diamond pasipo kutaja msanii huyo ameelekea wapi.
TUJIKUMBUSHE
Baada ya Diamond kumwagwa na Wema
mwishoni mwa mwaka jana, baadaye Februari mwaka huu, picha zilisambaa
kwenye mitandao ya kijamii zikimwonesha Dimpoz na Wema wakiwa kitandani,
hotelini nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini
viliandika kuwa wawili hao wana uhusiano wa kimapenzi huku ikielezwa
kwamba, uhusiano huo ulikuwepo kwa siri hata wakati Wema akiwa na
Diamond.
Hata hivyo, baadaye ikaja kuelezwa kuwa,
Wema na Dimpoz walikuwa nchini humo wakitengeneza video ya wimbo wa
Dimpoz uitwao Wanjera.

Note: Only a member of this blog may post a comment.