Thursday, September 17, 2015

Anonymous

Sheria ya Makosa Ya Mtandao Yanasa Watano Ambao Hutengeneza Message FEKI Za Wanasiasa!

Kamanda Kova
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii kufanya uhalifu wa  kutengeneza habari za uongo na uzushi dhidi ya viongozi au watu maarufu.

Akizungumza  na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova alisema watu hao wamekuwa wakitumia vibaya majina ya watu maarufu hasa wanasiasa.

Kova alitaja majina ya wanasiasa yanayotumiwa vibaya kuwa ni mgombea ubunge Jimbo la Kibamba, John Mnyika na mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na  usalama.

Aliwataja watuhumiwa hao, kuwa ni Joel Lumbay (32), Omar Suleiman wote wakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Michael Nickson (32) mkazi wa Tegeta, Patrick Natala  na Maxmillian Msacky wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Alisema watu hao, wamekuwa wakituma ujumbe mbalimbali  wakionesha viongozi hao walikuwa wanajadili jambo fulani dhidi ya kundi au chama  kingine cha siasa kwa kutumia mitandao.
“Wana tabia ya kutengeneza ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa lugha iliyozoeleka kama ‘kuchati,’  lakini mawasiliano hayo hayapo… yanakuwa yametengenezwa ili kutimiza malengo yao. Jambo hili ni kosa la jinai na linaweza kuchochea chuki  katika makundi ya watu,” alisema Kova.

Alisema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watu hao kwa kushirikiana  na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Kiongozi  au mtu yeyote atakayeona  ameathirika na mbinu  chafu za kihalifu  asisite kutoa taarifa kwa vyombo  vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,” alisema.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.