Wednesday, August 12, 2015

Anonymous

YANGA SC Yampa Beki Mrundi wa SIMBA SC Dau Mara Mbili


Beki wa kulia wa Simba Mrundi, Emily Namubona.
Sweetbert Lukonge,Dar es Salaam
YANGA wamezidi kuionea Simba katika usajili kwani hivi karibuni endapo uongozi wa Simba ungezubaa basi wangemsajili beki wao wa kulia, Mrundi, Emily Namubona.
Imefahamika kuwa Namubona alikuwa akiwindwa kwa udi na uvumba na Yanga ili aje kusaidiana Juma Abdul katika nafasi ya beki wa kulia.

Yanga ilikuwa ikimtumia mshambuliaji wake Amissi Tambwe, ambaye pia ni raia wa Burundi ili aweze kumshawishi beki huyo akubali kujiunga na Yanga.Akizungumza na Championi Jumatano, Namubona alisema aligoma kujiunga na timu hiyo kwa sababu tayari alikuwa ameshamalizana na Simba, hivyo akaogopa kuonekana tapeli.

“Kama ningekuwa na tamaa, basi ningeenda Yanga kwa sababu walinitangazia dau zuri kushinda lile nililokuwa tayari nimeshapewa na Simba, lakini sikutaka kufanya hivyo kwa sababu siyo uungwana. Yanga walitaka kunipatia dola 20,000 ikiwa ni mara mbili ya ile niliyopewa na Simba.

“Walikuwa wakiwatumia Tambwe pamoja na baadhi ya wachezaji wengine wa kikosi hicho ambao tunafahamiana, lakini niliwaambia siwezi kurudisha fedha za Simba kwa sababu tayari nilikuwa nimeshamalizana nao kwa kila kitu, kwani nikifanya hivyo nitaonekana tapeli na mimi sipendi niwe hivyo,” alisema Nimubona.
Mwaka 2012, Yanga ilitumia mbinu kama hiyo na kufanikiwa kuipiku Simba katika usajili wa Mbuyu Twite, ambaye ilijiunga na timu hiyo akitokea APR ya Rwanda.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.