Phillip Nkini Dar es Salaam
AKIWA na mwezi mmoja na nusu tu hapa nchini, Kocha wa Simba, Dylan Kerr, ameonekana kumfunika vibaya kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Hakuna ubishi kuwa Simba na Yanga ndizo timu zenye upinzani mkubwa sana hapa nchini na ndizo zinazoongoza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hakuna timu inayowafuatia hata kwa karibu.
Lakini takwimu za mwezi mmoja tu tangu Kerr, raia wa Uingereza alipojiunga na Simba, zinaonyesha ameweza kumaliza ubabe wa Pluijm, raia wa Uholanzi, ambaye ana uzoefu wa muda mrefu sana hapa nchini.
Hali halisi inaonyesha kuwa, tangu Kerr atue hapa nchini, amefanikiwa kuiongoza timu yake kucheza michezo sita ya kirafiki, huku Pluijm akiiongoza Yanga kwenye michezo saba tangu atoke mapumzikoni hadi siku ya Simba Day ambayo Msimbazi ndiyo walicheza mchezo wa mwisho wa sita.
Kwa kipindi hicho, Simba iliweza kucheza michezo ya kirafiki na timu za Polisi Zanzibar, Zanzibar Kombaini, KMKM, Black Sailor, Jang’ombe pamoja na Sports Club Villa.Yanga kwa kipindi hicho tangu Kerr atue hapa nchini, imeweza kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya KMKM pamoja na Villa, ukiachana na ile inayoendelea kucheza mfululizo jijini Mbeya ambayo inafanya iwe na idadi kubwa ya mechi zaidi ya Simba.
Kati ya michezo hiyo sita ya Yanga, mitano ni ya Kombe la Kagame ambayo ni dhidi ya Gor Mahia, KMKM, Al Khartoum, Telecom pamoja na Azam FC.
Ushindi:
Katika kipengele cha ushindi, Simba ya Kerr imeonekana kuwa juu pamoja na kwamba michezo yake ilikuwa ya kirafiki.
Simba imeweza kushinda michezo yote sita, ambapo ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Polisi Zanzibar, 2-1 dhidi ya Zanzibar Kombaini, wakaichapa KMKM mabao 3-2.
Pia walishinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Black Sailor, 3-0 dhidi ya Jang’ombe na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya SC Villa.
Kwa upande wa Yanga ambao wana michezo saba, wenyewe walipoteza michezo miwili na kutoka suluhu mmoja, walianza michezo ya kirafiki kwa kuichapa KMKM bao 1-0, baadaye wakatoka suluhu na SC Villa.
Walipoingia kwenye Kagame, walianza kwa kuchapwa mabao 2-1 na Gor Mahia, wakaichapa KMKM mabao 2-0, wakaifumua Telecom mabao 3-0, wakaipiga Al Khartoum ya Sudan bao 1-0, wakatoka suluhu na Azam lakini wakatolewa kwa mikwaju ya penalti.
Mabao ya kufunga:
Safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo inanolewa na Kerr, pia imeonyesha kuwa ipo imara zaidi ya ile ya Yanga iliyo chini ya Pluijm.
Simba kwenye michezo hiyo, imefunga mabao 16, huku Yanga wakiwa nyuma ya Simba mara mbili kwa kufunga mabao nane tu.
Kufungwa:
Yanga ya Pluijm hapa inaonekana kuwa na safu nzuri zaidi ya ulinzi, imeruhusu mabao mawili tu kwenye michezo yote saba, huku Simba ikiwa imeruhusu mabao matatu.
Hii inaonyesha kuwa safu ya ulinzi ya Yanga ambayo ipo chini ya Kelvin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, imeonyesha uimara zaidi ingawa ipo mbele mchezo mmoja.
Vinara wa kufunga:
Simba ya Kerr imeonekana kuwa na watu wengi ambao wanaweza kupachika mabao, tena mengi kwenye mechi moja.
Katika mabao yao 16, Simba wamefunga kupitia wachezaji sita tu, Ibrahim Ajibu na Elius Maguli ambao wamefunga manne kila mmoja, Mussa Mgosi na Hamis Kiiza wakifunga matatu kila mmoja na Awadhi Juma pamoja na Abdi Banda wakifunga bao moja kila mmoja.
Yanga wamefunga kupitia kwa Amissi Tambwe, aliyefunga mabao mawili, Donald Ngoma na Geofrey Mwashiuya wakifunga mojamoja, Malimi Busungu akafunga matatu, huku moja timu pinzani ikijifunga.
Kama kigezo ni za kirafiki:
Kama mtu atasema kuwa Simba walikuwa wanacheza michezo ya kirafiki, ukichukua michezo miwili dhidi ya Villa na KMKM, ambazo zilicheza na timu zote mbili, utakubali kuwa Simba ni zaidi.
Katika michezo hiyo ya kirafiki, Simba walishinda yote, huku Yanga wakitoka sare mmoja na kushinda mmoja.
Wednesday, August 12, 2015
Mzungu wa SIMBA SC, Kerr Amfunika Pluijm wa YANGA SC Vibaya!
USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK
TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)
Filed Under:
SPORTS AND ENTERTAINMENTS
on Wednesday, August 12, 2015
Note: Only a member of this blog may post a comment.