Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Aplina Philipo, MbeyaMASTAA wapya wa Yanga, Wazimbabwe Donald Ngoma, Thabani Kamusoko ‘Rasta’ na Mtogo, Vincent Bosou na jana walitandaza kandanda babkubwa wakati Yanga ikiizima Mbeya City kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa.
Hii ni mechi ya tatu Yanga inashinda mkoani hapa, ilianza kuichapa Kimondo 4-1, ikainyuka Prisons 2-0 na jana ikashusha kichapo hicho kwa City na kumuacha kocha Hans van Der Pluijm akichekelea kimoyomoyo. Yanga inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar.
Mabao ya Yanga jana yalifungwa na Andrey Coutinho, Amissi Tambwe na Ngoma, mabao ya City yalifungwa na Bakari Slane na Joseph Mahundi.
Ngoma alipiga bonge la bao kwa tik taka, akiunganisha krosi ya Tambwe. Bao hilo lilikuwa gumzo uwanjani. Ushirikiano wa Tambwe na Ngoma ulionekana kuwavuruga vilivyo City.
Beki Mtogo, Bossou alionyesha ubora wa hali ya juu kwa kuokoa mipira mingi ya hatari na kupandisha mashambulizi mara kwa mara.
Baada ya mchezo, Pluijm alisifia kikosi chake akisema kimecheza vizuri lakini kuna upungufu kidogo wa kurekebisha wakati Kocha wa City, Juma Mwambusi, alisema: “Sikutegemea kama kikosi kingefanya vibaya kulingana na maandalizi tuliyokuwa nayo, lakini imetusaidia kuona makosa na tutayafanyia kazi.”
Note: Only a member of this blog may post a comment.