Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr.
Wilbert Molandi, Dar es SalaamKOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ametangaza kuwa na majina tisa ya wachezaji wanaowania nafasi moja kwenye nafasi ya ushambuliaji, kati ya hao yupo straika mmoja wa Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Juzi Jumamosi, mashabiki wa Simba, walimshuhudia Mrundi, Kevin Ndayisenga, akicheza vyema kwenye pambano dhidi ya URA na kufunga bao moja wakati timu hiyo iliposhinda 2-1, lakini Kerr atakuwa na kazi kubwa, kwani kati ya orodha ndefu ya mastraika alionao, anahitaji mmoja tu ili kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni wanaotakiwa.
Tayari Simba ina wachezaji sita wa kigeni ambao ni beki Emir Namubona kutoka Burundi, Justice Majabvi (Zimbabwe), kipa Vincent Angban, raia wa Ivory Coast, Juuko Murshid (Mganda), Simon Sserunkuma (Mganda) na Hamis Kiiza (Mganda).
Katika kikosi chake, Simba ina washambuliaji watatu ambao ni mkongwe Mussa Mgosi, Kiiza na Ibrahim Ajibu na ikimnasa straika mwingine mmoja itakuwa imekamilika kila idara.
Orodha nyingine ya wachezaji wanaowania nafasi hiyo moja ni kutoka Rwanda, Kenya, DR Congo, Namibia, Zambia, Botswana, Msumbiji, Ghana na Afrika Kusini yenyewe.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kerr alisema tayari amefanya mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo kwa ajili ya kumsajili huku akiendelea kujiridhisha uwezo wake wa kufunga kwa kutumia mikanda ya video aliyotumiwa.
“Nimepokea maombi mengi ya mawakala kutoka nchi tisa hadi hivi sasa, wakiwataka wachezaji wake kuja kuichezea Simba baada ya kutangaza kuwa ninahitaji mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao.
“Kati ya maombi hayo, ninayafanyia kazi maombi ya mshambuliaji mmoja anayeichezea Orlando Pirates, jina lake ni siri kwa hivi sasa na nimepanga kulitangaza mara baada ya kumalizana naye,” alisema Kerr.
Ikumbukwe kuwa, Orlando Pirates imekuwa na urafiki wa muda mrefu na Simba.
Note: Only a member of this blog may post a comment.