Friday, August 14, 2015

Anonymous

VITA baridi ya CCM, UKAWA Haitatuacha Salama!

HISTORIA inatuonesha kwamba, kati ya mwaka 1945 na 1989, dunia iliingia kwenye mpasuko wa makundi hasimu mawili, yaliyokuwa kwenye Vita Baridi (Cold War) vilivyoanza mara tu baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945.

Upande mmoja ulikuwa na nchi zilizoshikamana na Marekani na Ulaya ya Magharibi na upande mwingine ulikuwa nchi zilizoshikamana na Umoja wa Kisovieti na Madola ya Ulaya ya Mashariki.

Pande zote zilijenga jeshi kubwa na kuwa na silaha nyingi lakini hazikuanzisha vita moja kwa moja, ingawa zilijaribu kutishana na kupeana matatizo kwa njia nyingi.

Kipindi hicho kilikuwa na maandilizi ya vita lakini vita ya kijeshi haikuanza. Sababu muhimu ya kutoingia kwenye mapigano ya wazi ilikuwa akiba kubwa ya silaha za nyuklia kila upande na wote walijua kwamba vita ingeleta uharibifu kwa nchi zote zilizoshiriki hata kwa dunia nzima.

Katika vita hiyo, Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza na Ufaransa zilikuwa nchi washindi wa vita hii dhidi ya Ujerumani. Urusi ilikuwa na Siasa za Kikomunisti lakini washindi wengine walifuata Siasa za Kidemokrasia na Uchumi wa Kibepari.

Nchi za Ulaya Mashariki na Ulaya ya Kati zilikaliwa na Jeshi la Kisovieti lililowahi kuwafukuza Wajerumani katika maeneo haya. Wasovieti walianza kuunda serikali zilizoshikamana nao mara nyingi kwa njia ya uchaguzi bandia na kwa kuwalazimisha wanasiasa wa nchi kama Poland au Hungary kutii madai yao.

Katika kila nchi, Chama cha Kikomunisti (Communist Party) kiliingizwa katika serikali na vyama vingine vya kisiasa na kuwekwa chini ya usimamizi wa Wakomunisti au Washauri Wasovieti.

Mwaka 1946, kiongozi Mwingereza, Winston Churchill alilalamika kwamba ‘zulia la chuma’ lilitandikwa katika Ulaya kuanzia Stettin, Upande wa Kaskazini hadi Trieste, Upande wa Kusini na nyuma yake uhuru ulikandamizwa.

Kama ulivyo usemi kwamba wapiganapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi, ndivyo ilivyokuwa kwa maendeleo ya Afrika kwani yaliathiriwa vibaya na vita hiyo.

Kwa jumla kila upande ulijaribu kuvuta nchi changa za Afrika upande wao. Kama serikali ilipatana na upande mmoja, upande mwingine mara nyingi ulikuwa tayari kusaidia wapinzani wa ndani kwa msaada wa silaha na fedha.

Wapigania uhuru katika Koloni za Ureno kama Msumbiji walipata msaada wa silaha kutoka nchi za Mashariki. Wapinzani hao walitazamiwa na Magharibi kama Wakomunisti na wakala wa Wasovieti hivyo Marekani ilisaidia Afrika Kusini, ingawa siasa za ubaguzi wa rangi zilivunja haki za kidemokrasia.

Madikteta wengi wa Afrika walipata usaidizi wa upande mmoja au mwingine wakitangaza tu kushikamana nao.

Hata kama serikali fulani ya Afrika iliharibu uchumi na kuvunja haki za binadamu, iliweza kutegemea usaidizi kutoka kwa upande mmoja wa vita baridi ikijitangaza iko upande wao hivyo kusababisha mgawanyiko na kuvuruga utawala uliokuwepo.

Hicho ndicho kinachoonekana katika vita ya maneno ya makundi mawili ya wagombea Urais nchini Tanzania. Kundi la mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli na lile la mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa.

Ifahamike kwamba, mbali na Magufuli na Lowassa, hakuna mgombea mwingine anayeweza kuleta changamoto ya kuwazidi wawili hao.

Tayari makundi haya mawili yapo vitani. Uzuri ni vita ya maneno (baridi) na Watanzania wangeomba iendelee hivyohivyo hadi fainali ambayo ni Oktoba 25, mwaka huu.

Tumewasikia CCM wakimuita Lowassa na wenzake waliokihama chama hicho kuwa ni makapi. Kwamba wao wana mgombea wakati Ukawa wana kapi.

Kama hiyo haitoshi, tumewasikia wakisema Lowassa ananunua urais wakati enzi akiwa CCM hawakuthubutu kumtuhumu kwa jambo hilo. Leo kwa kuwa yupo upande wa pili basi wanamtuhumu kwa kashfa kedekede.

Naye Lowassa akashindwa kuvumilia. Akajibu mapigo. Kwamba, CCM ndiyo waliowafanya Watanzania wawe maskini. Ndiyo waliowafanya Watanzania wateseke na hali mbaya ya maisha. Ndiyo kwanza vita imeanza hata kabla ya kampeni zitakazopulizwa kipyenga Agosti 22, mwaka huu.

Kama tulivyoona madhara ya Vita Baridi kwa nchi zinazoendelea, je, Watanzania tumejiandaaje kwa madhara ya vita hii ya CCM na Ukawa? Kwamba, maisha yatakuwaje baada ya uchaguzi, iwe CCM imeshinda au Ukawa imeshinda?

Japokuwa wagombea wanasema watafanya kampeni za kistaharabu zisizokuwa na fujo lakini mpasuko wa pande mbili katika jamii yetu haufichiki.

Mgawanyiko wa CCM na Ukawa ni dhahiri kwamba, hautaacha usawa kwa wakulima, wafanyakazi, wafanyabishara na makundi mengine. Je, vipi kuhusu usalama na uchumi wa Mtanzania? Tukifikia hatua hiyo, kama hakutatokea mtu wa kuwatuliza Watanzania na kuwarudisha pamoja, utawala wa nchi hii utakuwa mgumu. Tumejiandaaje?

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.