Wednesday, August 5, 2015

Anonymous

OKWI, KIIZA Wamchongea Aucho YANGA SC

IMG_5609
Hans Mloli, Dar es Salaam
DILI la usajili la kiungo wa Gor Mahia ya Kenya, Mganda, Khalid Aucho kutua Yanga linaweza kuishia gizani baada ya kuingia doa kutokana na taarifa za wachezaji wengine wawili Waganda, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza waliowahi kuitumikia Yanga kipindi cha nyuma.

Imeelezwa kuwa ingawa benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha Mdachi, Hans van Der Pluijm lilikubali kiwango cha Aucho alichokionyesha kwenye michuano ya Kombe la Kagame, lakini baadhi ya viongozi wa Yanga hawajakubaliana na suala hilo kwa kuhofia kurejesha tatizo la utovu wa nidhamu uliowahi kuonyeshwa na Okwi na Kiiza ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.

Kwa muda mrefu tangu Okwi akiwa Simba SC mpaka anatua Yanga kuungana na Kiiza, wachezaji hao wamekuwa wakilalamikiwa kwa tabia za utovu wa nidhamu, majivuno na kuchelewa kurejea nchini wanapokwenda nyumbani kupumzika, hivyo mwenendo huo umewatia hofu viongozi wa Yanga kuhusiana na Aucho kwa kigezo kuwa wote wanatoka taifa moja.

“Kila mmoja anafahamu kuhusiana na usumbufu wa wachezaji wa Uganda wanapokuja kucheza soka nje ya nchi, wengi walishuhudia usumbufu wa Kiiza na Okwi inapotokea wamemaliza mapumziko na wanahitaji kurudi kuendelea na majukumu.

“Hilo hatuhitaji lijirudie tena, ndiyo maana hata huyu Aucho itatupasa kuwa makini katika usajili wake kama mwalimu ataonyesha dhati ya kumhitaji, lazima tukae tushauriane kwa kina maana ni jambo ambalo linahitaji umakini kabla ya kufanya maamuzi.

“Yanga kwa sasa imetulia na kama kutaibuka mambo kama hayo msimu ujao halitakuwa jambo jema. Ila haya yote tutayafahamu baada ya kukutana na uongozi kuangalia ripoti na maagizo ya mwalimu alichokiona kwenye Kagame, kisha baada ya hapo tutajua itakavyokuwa,” alisema kigogo mmoja wa Yanga.
Pamoja na hayo, lakini imekuwa ikiripotiwa kuwa Yanga imevutiwa pia na uwezo wa kiungo wa Al Khartoum ya Sudan, Anthony Akumu na yule wa Platinum, Thabani Kamusoko.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.