Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
Mshituko mkubwa
umewakumba wakazi wa Kijitonyama Kwaally Maua B, wilayani Kinondoni
jijini Dar es Salaam baada ya Ijumaa kuamkia Jumamosi iliyopita kuibuka
kwa ugonjwa wa ajabu ulioua watu wawili ghafla na kuwapa hofu kubwa
wakazi wa eneo hilo.
Timu ya Uwazi baada ya kuarifiwa juu ya tukio hilo, ilifika katika eneo hilo na kukuta wafiwa wakilia huku wagonjwa wengine wakikimbizwa hospitalini.
Katika mahojiano na mjumbe wa shina
namba 19 wa eneo hilo, Mohamed Juma Ngaopera alisema tatizo hilo
lilianza Ijumaa iliyopita saa 3.30 usiku.
“Ugonjwa huo ukaenea eneo hili na
waliokuwa wakikumbwa tukawa tunawakimbiza hospitalini lakini mtu mzima
mmoja naye akafariki hivyo, mpaka sasa watu wawili wameshapoteza
maisha,” alisema kiongozi huyo.
Alipoulizwa chanzo, alisema hawajui kwa
sababu haujabainishwa kitaalamu na amewataja waliopeteza maisha kuwa ni
Zawadi Kipepe (5) na Abas Hussein (50).
Alisema
baadhi ya wagonjwa waliokumbwa na maradhi hayo na wanaendelea na
matibabu ni pamoja na Ramadhan Hussein, Shaban Hussein, Saum Kipepe,
Idrisa Kipepe, Morina Mohamed wote wamelazwa Hospitali ya Parestina,
jijini Dar.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa, baada ya
kuona hali inazidi kuwa mbaya waliomba msaada Halmashauri ya Jiji ambao
walifika na kupuliza dawa eneo hilo kisha kufunga nyumba ambazo wagonjwa
hao walikuwa wakiishi ili uchunguzi zaidi ufanyike.
Hata hivyo, mmoja wa maafisa wa afya wa
jiji waliofika eneo hilo alipoulizwa na waandishi wetu kama dalili za
ugonjwa huo ni za kipindupindu, kwa sharti la kutoandikwa jina kwa kuwa
siyo msemaji, afisa huyo alisema:
“Kinachoonekana hapa si kipindupindu
bali kuna uhasama kati ya familia moja na nyingine. Kwa nini tatizo
hilo liikumbe familia moja tu?”
Note: Only a member of this blog may post a comment.