TATHMINI YA WATU WALIOHUDHURIA
Katika kile kilichotajwa kama zaidi ya mafuriko, ‘Tsunami’, umati
uliohudhuria tukio hilo unakadiriwa kufikia maelfu kwa maelfu wakiwemo
wananchi mbalimbali, wanachama wa CCM na wasanii mbalimbali wa muziki wa
zamani na wa kizazi kipya, wamkiwemo waigizaji.
Wasanii waliokuwepo ni pamoja na Nasibu Abdul ‘Diamond’, Khadija Kopa akiwa na Kundi la Tanzania One Theatre, Yamoto Band, Steve Mengele ‘Steve Nyerere’, Single Mtambalike ‘Rich’, Wema Sepetu aliyeambatana na Yobnesh Yusuph ‘Batuli’, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, Khalid Ramadhani ‘Tunda Man’, Astelina Sanga ‘Linah’ na wengine kibao ambao baadhi yao walionesha uwepo wao kwa kutumbuiza nyimbo mbalimbali jukwaani.
MAMBO YAANZA
Ishu nzima ilianza saa 7 mchana ambapo wasanii mbalimbali walipanda
jukwaani kutoa burudani likiwemo kundi la TOT, Vijana Jazz, Bendi ya
Walemavu na wakafuatiwa na Yamoto Band kisha msanii wa Mnanda, Easy Man,
Bushoke na akaingia Peter Msechu. Baadaye ilikuwa ni zamu ya Rais wa
Wasafi, Diamond ambaye alifunga duru kwa upande wa burudani huku shoo
yake ikinogeshwa na gwiji wa komedi nchini, Amri Athman ‘Mzee Majuto’.
Baadhi ya wasanii walitia fora kwa kubadili nyimbo zao na kuwa zenye
kukisifia chama hicho ambapo, Diamond aliubadilisha wimbo wake wa Number
One, Yamoto Band nao waliubadilisha wimbo wao wa Niseme Nisiseme.
Halikadhalika Peter Msechu ambaye aliubadili wimbo wake wa Nyota.
SALAMU ZA WAWAKILISHI
Baada ya burudani, Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho, Nape
Nnauye aliwakaribisha baadhi ya wawakilishi kutoka vyama vya siasa, na
makundi mbalimbali ya kijamii ambapo wafanyabiashara ndogondogo
‘Wamachinga’ nao walitoa salamu zao kupitia kwa mwenyekiti wao huku
waendesha pikipiki ‘bodaboda’ nao wakiwakilishwa na mwenyekiti wao.
Mmoja wa watangaza nia ambaye naye alikatwa katika kinyang’anyiro cha
urais wa chama hicho, Makongoro Nyerere ambaye alipewa nafasi ya
kuwakilisha familia ya muasisi wa taifa la Tanzania, Baba wa Taifa,
Hayati Julius Nyerere, alionekana kuwa kivutio kutokana na vijembe
mbalimbali alivyowapiga Ukawa.
“Tutawapiga tobo si wametaka wenyewe, maana kama mzee kaingia mchezo
wa vijana mnategemea mimi nifanyaje! Nitampiga tobo na akigeuka
nitampiga kanzu. Miwani Oyeeee, Kofia Oyeeee, Kifimbo oyeee,” alisema
Makongoro na kuamsha shangwe ya kutosha kutoka kwa wana- CCM.
Baadhi ya viongozi waliofanikiwa kutoa salamu zao ni, Waziri Mkuu
Mstaafu (Jaji Joseph Warioba), Rais Mstaafu Awamu ya Pili (Ali Hassan
Mwinyi), Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu (Benjamin Mkapa), Katibu Mkuu wa
CCM (Abdulrahman Kinana) na kumaliziwa na Rais Jakaya Kikwete.
MKAPA AWAPA MAKAVU LAIVU
Katika hatua nyingine, rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwapa ‘makavu
laivu’ Ukawa akisema ni watu wasiokuwa na hoja katika siasa ya vyama
vingi na wamejaa uchu wa madaraka huku Jaji Warioba yeye akimmwagia sifa
kibao mgombea wa chama hicho, John Magufuli ‘JM’.
Naye John Magufuli ambaye ndiye mlengwa wa uzinduzi huo, alifungua
kampeni zake kwa kutoa ahadi kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo
kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji huku akilenga kufanya
mabadiliko kwa walimu, mama lishe, wafanyabiashara ndogondogo,
wanafunzi, hasa suala la mikopo na suala la ajira sambamba na
kumtambulisha mke wake, Janet Magufuli.
Katika uzinduzi huo aliyekuwa mgombea wa Chadema katika Jimbo la
Sikonge, Said Nkumba alirejea CCM ikiwa ni siku chache alipotangaza
kujiunga na chama hicho cha upinzani.
Stori: Richard Bukos, Gabriel Ngo’sha, Chande Abdallah, Deogratius Mongela na Shani Ramadhani.

Note: Only a member of this blog may post a comment.