ILIPOISHIA
WINGI wa simu na sms
ninazotumiwa na wasomaji wetu wapendwa, hakika zinathibitisha ni kwa
namna na jinsi gani simulizi hii tamu ya maisha ya JB inavyowagusa watu
wengi. Hakika ni simulizi ambayo hata mimi, wakati naandika huwa
najikuta nasisimka kwa jinsi inavyonipa somo na mambo mengi sana ya
kujifunza.
Ni mfululizo wa maisha yake,
tangu kuzaliwa hadi alipo sasa. Ni mengi amepitia, yenye furaha, huzuni,
uchungu, faraja, maumivu na kila aina ya misukosuko ya maisha. Wiki
iliyopita, tuliishia pale alipoweka wazi orodha ya wasanii wanaoongoza
kwa ‘kufukia msosi’. Twende pamoja…
“Kwa hiyo mambo ya kutamani sana kuwa staa siyo mazuri kabisa, kabisakabisa, ni maisha ya taabu na mabaya mno,” anasema JB. “Eeeh, nasema ni maisha ya taabu kwa sababu wewe hapo Masalu, unaweza kutembea barabarani huku ukila mhindi au hata muwa, lakini mimi nikifanya hivyo, watu watashangaa na kuanza kuzua maneno mengi, tena inakuwa habari na kwenu waandishi, kwa hiyo maisha ya kujulikana sana siyo ya kutamani, unakosa uhuru wa kufanya baadhi ya mambo yako,” anasema mfululizo bila kuweka nukta huku akihema kwa nguvu.
“Mmh, ikawaje kaka?,” namuuliza kwa shauku kubwa ya kutaka kujua kwa undani zaidi juu ya simulizi na maisha yake kwa ujumla.
“Kwa hiyo nikawa nimeachana tena na mambo ya kuigiza, nikajikita kwenye biashara zangu ikiwemo za kuuza mahindi, kama nilivyokwishaeleza huko nyuma.”
“Kwa hiyo Richie hakukusumbua tena ulipoacha?,” namtupia swali huku nikimtazama machoni.
“Hakunisumbua kabisa, unajua wakati huo naye alikuwa ‘bize’ na mambo yake, kwa kipindi hicho alikuwa akifanya kazi kwenye kiwanda cha chai cha Chai Bora, kwa hiyo hakunisumbua tena,” anabainisha JB.
“Basi, mwanzoni mwa mwaka 2000, alinifuata msanii mmoja ambaye jina lake halisi ni George Paul, lakini jina maarufu ambalo linajulikana kwa wengi ni la Mjomba Fujo, huyu jamaa alikuja na wazo la kuanzisha kampuni ya uzalishaji wa filamu,” anasema JB.
“Nikawa na wasiwasi sana juu ya wazo hilo, kwa sababu kipindi hicho hakukuwa na mwamko sana kwenye mambo ya sanaa hapa nchini, kwani hata filamu zilizokuwa sokoni zilikuwa zinahesabika sana,” anasema JB huku akiangaza huku na kule kama anayetafuta kitu muhimu sana.
“Vipi kaka, mbona kama umehamisha tena mawazo hapa?,” namuuliza kwa sauti ya upole kabisa.
“Si huyu msichana wa chakula, njaa inaanza kunisakama na nikiwa na njaa huwa siwezi kuongea kabisa, lakini ngoja tuendelee bwana,” anasema huku akikohoa.
“Baada ya kutafakari kwa kina na kwa muda mrefu sana, hatimaye nilimkubalia Mjomba Fujo juu ya wazo lake la kuanzisha kampuni, kwa hiyo kwa pamoja na ushirikiano mkubwa kabisa, tukaanzisha kampuni ya Jerusalem, hata hilo jina ni yeye (Mjomba Fujo) aliyelitoa,” anasema JB.
“Tukiwa na moto wa kuanzisha kampuni, hapohapo tukaigiza sinema moja ambayo tuliipa jina la Kanisa la Leo, lakini ilichelewa sana kuingia sokoni, hali ikabadilika tena,” anasema na kuchukua glasi ya maji na kuisukumizia kinywani kwa fujo.
“Ikawaje?,” nikamuuliza.
“Mjomba Fujo alikata tamaa kabisa baada ya sinema ile kuchelewa kuingia sokoni, nadhani wakati anakuja na wazo la kuanzisha kampuni ya kutengeneza sinema, alikuwa akitarajia kupata pesa za haraka sana,” anasema.
“Kwa hiyo akawa ameondoka kwenye kampuni na kuniacha peke yangu, na mimi nikaamua kukomaa, nikajiapiza sasa filamu iwe kazi yangu ya kwanza na muhimu maishani mwangu,” anasema JB.
“Kabla hiyo sinema ya Kanisa la Leo haijatoka, nikatengeneza tena sinema ya Agano la Urithi, ambapo nilionesha kiwango cha juu sana katika uigizaji,” anasema huku akiegemea kiti chake na kunyoosha miguu kabla ya kupiga miayo na kufunika kinywa kwa kiganja chake cha mkono wa kushoto.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatillia wiki ijayo kwa uhondo zaidi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.