Tuesday, August 18, 2015

Anonymous

HUU NDIO UKWELI: Atakayekwenda Ikulu ni Mmoja Wengine Tutabaki Uswazi

magufuliUKIPITA mitaani siasa zimepamba moto, mabishano baina ya makundi hasimu yatokanayo na wagombea wa nafasi ya urais hivi sasa ni sawa na vita! Kila unayemsikia hushindwi kuamini kuwa naye ni miongoni mwa watakaoingia ikulu endapo mgombea wake atashinda.
lowassa2.jpg“Mwaka huu hatukubali, kwa namna yoyote lazima kieleweke, tumechoka.” Haya si maneno ya shabiki wa siasa, ni ya msafiri aendaye ikulu baada ya uchaguzi, lakini je, ni kweli kwamba Watanzania wote milioni 45 baada ya uchaguzi wataishi ikulu, wale na kunywa mvinyo chini ya uangalizi wa madaktari bingwa?
Jibu si la kutafuta zaidi ya ‘hapana.’Ikiwa hivyo ndivyo, mzuka wa wananchi wa kawaida waishio uswazi, namaanisha uswahilini, unatoka wapi ilhali wao siyo miongoni mwa waendao ikulu baada tu ya ushindi kupatikana Oktoba 25, mwaka huu?

Ukweli ni huu, wananchi wamebinafsisha maisha yao kwa wagombea, hivi sasa wanaishi kwa matumaini. “Akishinda fulani atasaidia kutuondolea maisha ya shida.”

Kwa mdadisi kama mimi siwezi kupuuza matarajio hayo ya wananchi walio wengi hivi sasa mitaani, pengine shaka yangu ni kwamba lini hizo shida zitaondolewa miongoni mwao na huyo wanayemtarajia aingie ikulu awakomboe?

Niliwahi kuandika katika moja ya makala zangu kuwa umaskini siyo jiwe linalohitaji mtu mwenye nguvu kulitwaa na kulitupa baharini na kesho yake nchi nzima ikaamkia kwenye utajiri, ni mchakato mrefu unaohitaji muda na uvumilivu kuukamilisha.

Kwa sababu hiyo sitarajii kuwaona wananchi wa kawaida wakiweka nadhiri kubwa za kuhakikisha mgombea wao anashinda kana kwamba ukomo wa tabu zao ni baada ya Oktoba 25.

Lazima tukubaliane kuwa, anayekwenda ikulu ni mmoja wengine tutabaki uswazi tukipepeta dengu hata baada ya mshindi kupatikana.

Ni vema nikasema; mwenye uhakika wa kulala na kuamka katika maisha mengine ni mshindi wa nafasi ya urais. Huyu ndiye anayeweza kulala Tandale, Magomeni jijini Dar es Salaam na siku akishinda anaamkia ikulu akilindwa na maofisa usalama wa taifa.

Mbali na huyo wengine wote tutabaki tulipo, tutalala kwenye vitanda vilevile, tutajifunika shuka zilezile, majirani zetu watabaki kuwa walewale na hali ya maisha yetu itabaki katika mazoea yaleyale.

Ikiwa ni hivi; wananchi wenzangu tuna kila sababu kuhakikisha kuwa pamoja na ushabiki wetu, hatuvurugi maisha yetu, hatuharibu uhusiano na mshikamano tulio nao kwa sababu ya kuwasapoti waenda ikulu ambao naamini kwa misingi ya uzoefu, hawajawahi kuwa msaada wa moja kwa moja kwenye maisha ya watu wa kawaida baada ya kushinda kwao.

Tukumbuke; ushindi wa mgombea urais kwa uadilifu na sifa zozote alizonazo ni mchakato wa kuijenga Tanzania mpya siyo hii tuliyonayo.

Ikiwa tumebinafsisha maisha yetu kwa wagombea hawa kwa imani kuwa watatuondolea shida za leo, hilo litakuwa gumu kutekelezeka kisayansi kama nilivyosema.

Nashauri; tusijenge maisha ya wagombea urais kwa kuharibu mfumo wetu wa amani ya nchi ambao ndiyo utakaowasaidia hao wanaotaka kutuongoza kutupatia maisha mapya, vinginevyo kwenye machafuko na vita hata akitawala nabii hataweza kubadilisha sura ya nchi.

Nahitimisha uchochezi wangu kwa kuwaomba Watanzania wote pamoja na vuguvugu la kisiasa lililopo mwaka huu, tusijisahau kulinda amani yetu kwa ajili ya faida ya taifa la leo na kesho.

Kidumu Chama Cha Mapinduzi, udumu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini taifa letu lidumu zaidi na zaidi. Nachochea tu!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.