Deogratius Mongela na Chande Abdallah
WIKI hii Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers kwa mara nyingine ilitimba eneo la kibiashara la Mlimani City jijini Dar ikiwa na mfano wa silaha aina ya bastola ‘toy’ ili kupima ulinzi kwenye eneo hilo kufuatia matukio mbalimbali ya uvamizi wa kutumia silaha na ugaidi ambapo ilibaini kuwa ulinzi ni hafifu. OFM ilitimba eneo hilo baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa ulinzi hafifu hasa katika eneo la kuingia ambapo utaratibu ulionesha kuwepo kwa ukaguzi wa juujuu kwa wanaoingia kwa magari huku watembea kwa miguu wakiingia bila kukaguliwa.
OFM iliingia mzigoni ili kupata ukweli kuhusu usalama wa eneo hilo huku wakiwa na ‘silaha’ hiyo ambayo mmoja wa makamanda wa OFM aliibeba na kupita maeneo yote ya ulinzi, lakini pamoja na uwepo wa askari wengi kwenye eneo hilo ilikuwa kazi rahisi kurandaranda sehemu mbalimbali.
Maeneo ambayo yalifikiwa na OFM ni yale yenye mkusanyiko wa watu na muhimu kama vile benki, madukani, supermarket na hata sehemu za faragha kama vyooni ambapo aliweza kubadilisha ‘silaha’ yake kutoka mfuko mmoja na kuiweka mwingine.
Kamanda huyo, huku akipigwa picha na mwenzake kila eneo alilopita alitumia saa mbili kupita sehemu mbalimbali ambapo katika moja ya maeneo alipishana na askari wanaolinda baadhi ya maduka yaliyomo ndani na kusimama eneo moja kwa zaidi ya robo saa, akiwasiliana kwa simu lakini hakushtukiwa chochote na walinzi.
Mpaka makamanda hao wanaondoka eneo hilo, hakukuwa na dalili zozote zilizoonesha kuwepo kwa usalama wa kutosha hasa kwa baadhi ya watu ambao walionekana wakiingia na mizigo mbalimbali bila kukaguliwa.
Baada ya kubaini hatari hiyo, gazeti hili lilizungumza na mmoja wa maafisa wa ulinzi ambaye aliomba hifadhi ya jina ambapo alieleza kwamba, katika eneo hilo hakuna ulinzi wa mtu binafsi ila kipindi cha nyuma ulikuwepo kwa sababu ya tishio la ugaidi wa Al-Shabaab kama ilivyotokea nchini Kenya kwenye Maduka ya Westgate.
Hii siyo mara ya kwanza kwa OFM kubaini udhaifu wa ulinzi katika jengo hilo kwani mwaka juzi OFM waliripoti tukio kama hilo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.