Leo kwenye safu hii mwanadada Wastara Juma yupo hapa kujibu maswali 10 aliyoulizwa na Mwandishi Wetu Imelda Mtema. Unataka kujua kaulizwa nini na akajibu nini? Fuatilia hapa chini…
Ijumaa: Hivi ulipopata kilema cha kukosa mguu mmoja wakati ulishazoea kutembea na miguu miwili ulijisikiaje?
Wastara: Nakumbuka nilipoteza matumaini kabisa na kuona ndoto zangu zimefutika.
Ijumaa: Changamoto gani ulikutana nazo tangu ulipopata ulemavu?
Wastara: Ni nyingi
sana, kwanza kubadili aina ya mwendo wakati watu walizoea kukuona
ukidunda. Kifupi wengi walinishangaa kwa jinsi nilivyoanza kutembea,
pilika za kimaisha kama utafutaji pia vilinifanya nipate changamoto
kubwa kwani sikuwa nikisaidiwa.
Ijumaa: Uliwezaje kukabiliana na badiliko kubwa kama hilo katika mwili wako?
Wastara: Ilikuwa kazi
kubwa sana kuzoea hali hii maana nilikuwa naanguka kila siku kwa
kujisahau na kuona bado nina miguu yote. Kutokana na hali hiyo
nilichelewa sana kupona mpaka daktari aliyekuwa ananitibu akaamua kunipa
dawa ambazo zilinifanya nilale saa 24.
Ijumaa: Ulemavu wako haukupi mawazo hasa unapofikiria ishu ya kuolewa tena?
Wastara: Hili suala la
kuolewa ndiyo gumu kabisa na naweza kusema ulemavu huu unanikosesha hamu
ya kuolewa kwani kila mwanaume anayekuja naona hana mapenzi ya kweli na
mimi, naamua kughairi.
Ijumaa: Uliwaza nini kuamua kugombea ubunge na hiyo hali yako?
Wastara: Nimefikiria vitu vingi sana na lengo ni kuwasaidia walemavu kwa kila hali.
Ijumaa: Wewe ulishawahi kunyanyapaliwa kutokana na hivyo ulivyo?
Wastara: Nilishawahi
kwani nakumbuka siku moja nilitembelea nchi fulani nikapewa chumba
nilale na mwenyeji wangu lakini alipoona ni mlemavu alihama.
Ijumaa: Ni maumivu gani uliyoyapitia kwa kipindi chote hiki?
Wastara: Kubwa zaidi ni maumivu ya mwili kwani kuvaa mguu wa plastiki ni mateso makubwa asikwambie mtu.
Ijumaa: Ni yapi umepanga kuyafanya kwenye siasa?
Wastara: Kwanza nitahakikisha serikali inaweka huduma nzuri hospitalini, benki na kwenye mabasi kwa walemavu.
Ijumaa: Je, umejipangaje katika kuikabili mizengwe kwenye siasa?
Wastara: Siasa siiogopi, nimejipanga kwa kila kitu na watu wasubiri waone.
Ijumaa: Huogopi mchezo mchafu unaofanywa na wanasiasa?
Wastara: Hakika nimejipanga na niko tayari kukabiliana na changamoto zote.


Note: Only a member of this blog may post a comment.