Friday, July 24, 2015

Anonymous

MAKAVU LIVE! SHAMSA FORD, BOZI...KUSHOBOKEA WENYE NAZO KUTAWATOKEA PUANI!

KUNA muigizaji mmoja mkubwa nafahamu sana uwezo wake na katika siku za hivi karibuni, amekuwa akinivutia baada ya kumtazama katika kazi zake kadhaa, Shamsa Ford. Halafu kuna huyu mwingine, Fatma Ayoub maarufu kama Bozi, naye anajitahidi kiasi chake.

Kwa nyakati tofauti wametoa kauli zilizonifanya nifikirie mara mbilimbili; kwamba wao wanahitaji kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume wenye nazo, kwa sababu hawa akina pangu pakavu tia mchuzi, ni pasua kichwa!
Shamsa, ambaye kwa mara ya mwisho nilifahamu akitoka na Nay wa Mitego, amesema ameumizwa mara nyingi katika mapenzi na mbaya zaidi wanaomuumiza hawana pesa, hivyo ameona ni bora tu akaamua kuwatafuta vibopa ili hata kama atapata ma-stress, yawe na sababu!

Kimsingi, ni haki ya msingi ya kila mtu kuamua aina ya maisha anayotaka kuishi, kwa sababu ana sababu zake. Hii siyo dhambi wala uvunjivu wa sheria. Yaani akitokea mtu akaamua kwa hiyari yake mwenyewe kuvua viatu na kuingia chooni pekupeku kila anapojisikia haja, utakuwa mtu wa ajabu ukienda kumshtaki!

Shamsa na Bozi wanapoamua kutaka wanaume wenye fedha ili washiriki nao mapenzi ni sawa tu na wanawake wanaopenda ngono zembe na bila kuchagua wala kujali hela, kwa sababu hicho ndicho roho yao inapenda. Ulimwengu utakushangaa endapo utakuja juu ukilalamikia kitendo hicho!

Lakini ipo tofauti kati ya nani anayefanya hivyo. Kwa mfano, leo hii akitokea bwana afya, akawa ndiye anayekwenda chooni bila viatu, lazima tutapaza sauti ya mshangao, kwa sababu tunaamini huyu wajibu wake ni kutuhimiza kuvaa viatu wakati wa kwenda chooni ili kujilinda na maambukizi ya vijidudu vya maradhi!

Hivi ndivyo ilivyo kwa wasichana hawa, hasa Shamsa, ambaye miongoni mwa mashabiki wake ni watu wazima wenye busara zao, ambao hawawezi kupendezwa kusikia maneno kama haya yakitoka mdomoni mwake.
Inawezekana anahitaji mwanaume mwenye fedha, kwa sababu labda hela ndiyo kila kitu, lakini unapofikia wakati wa kuhitaji mtu anayeitwa mume, fedha siyo kigezo nambari wani. Na mara nyingi, kama hajui, ndoa nyingi za wanaume wenye fedha zinaongoza kwa maudhi, mifarakano na ukosefu wa amani.

Kama ishu ni mwanaume mwenye fedha, je, hela za kiwango gani? Maana kuna wanaume wengi wenye fedha, lakini zinatofautiana. Hofu yangu anaweza kugeuka mpira, kila mchezaji anaupiga.

Lakini achana na hofu ya wao kuwa mpira, pia kuna ishu ya uadilifu. Staa kama Shamsa, muigizaji mwenye weledi, kutoa maneno haya kunasapoti moja ya mashairi ya Nay wa Mitego katika moja ya nyimbo zake kuwa ukitaka akina dada wanaojiuza, lakini wenye viwango, nenda Bongo Movie. Ni kweli?

Huwezi kuondoa stress za maisha kwa kuishi na mwanaume mwenye fedha, isipokuwa utaziongeza na pengine kukupa msongo wa mawazo kabisa. Huenda wametoa kauli hiyo bila kujua, lakini ina madhara makubwa.
Tunatofautiana mtizamo, kwangu mimi naweza kufikiri wanawaalika wenye nazo. Hawa watakuwa wangapi? Kwake yeye, fedha ndicho kitu cha muhimu, hajali utu, upendo wala staha yake kama mwanamke.

Tunapokuwa na mastaa wenye mtazamo kama huu, tunakosa nguvu ya kuwatetea wanapofikwa na matukio ya kimapenzi kwa makosa ya wenza wao. Hivi unategemea nini leo hii, msichana anayejinadi kutaka fedha kwenye mapenzi, tukisikia kafikwa?

Na tatizo moja la wanaume ni kuwa wanapokutana na mwanamke anayetanguliza mbele masilahi, huwa hawana heshima kwake, zaidi ya kutaka hata kumdhalilisha, ili mradi tu kumkomesha.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.