Lakini pia wapo ambao mpaka leo hii unavyowaona, wameachwa na kuacha sana. Hilo linatufanya tuamini kwamba kuachana ni jambo la kawaida. Siyo ajabu wewe kuachana na huyo uliyenaye kwa kuwa utakuwa si wa kwanza kuacha wala kuachwa.
Wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo watu ni wa ajabu sana na naweza kuwaita washamba waliopitiliza. Hivi karibuni nikiwa napitiapitia mtandao wa Facebook, nilishangazwa na post ya rafiki yangu mmoja akimchamba mpenzi wake aliyemuacha.
Rafiki yangu huyo aliachwa baada ya kufanya usaliti. Yaani kwenye simu yake zilikutwa meseji za kimahaba alizomtumia msichana mwingine. Msichana akakasirika, akaona amwage uchafu wa mpenzi wake huyo kwenye mtandao.
Katika kujibu mashambulizi, yule rafiki yangu akaanza kuandika mambo kibao machafu ya demu wake huyo huku akiambatanisha na picha. Aliandikaje? Soma hii aya moja ifuatayo;
“Nimekuvumilia kwa mengi, mara ngapi nimekufumania nikakusamehe? Halafu wewe ni mwanamke gani usiyejua mapenzi, nani asiyejua kuwa wewe ni mchafu? Nimekuvumilia kwa mengi lakini kiukweli wewe hukustahili kuwa na mimi.”
Hebu vuta picha, hayo ni maneno anayoandika mwanaume kwa mpenzi wake ambaye wamedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Nilipigwa na butwaa lakini nikaona ni vyema nikaandika hapa ili angalau kuonesha kuwa hili si jambo linalofaa kwenye ulimwengu wa mapenzi wa watu waliostaarabika.
Ukweli ni kwamba, kwa mtu ambaye mmekuwa pamoja kwenye uhusiano, hata yatokee yapi, jaribu kujizuia kuachana naye kwa ubaya, ikitokea hivyo, basi tusiwe wepesi wa kukimbilia kuanika mabaya ya wapenzi wetu wa zamani.
Hivi hata kama ni wewe, umeachana leo na mpenzi wako kisha kesho unasikia anakusambazia habari zako mbaya, utajisikiaje?
Utamsikia mtu akisema, ‘Ooh, yule muone hivi hivi, ana wanawake kibao, mwanamke wa kuwa naye yule awe tayari kusalitiwa.’ Huyo ni msichana anamsema vibaya mpenzi wake wa zamani. Kwa nini anafanya hivyo? Eti anaamini atakuwa amemkomoa na kumchafua.
Ukifuatilia unaweza kubaini kuwa, mwanaume hana tabia ambazo mpenzi wake anazinadi, sasa unajiuliza kwa nini mtu afikie huko? Kama kakuacha ni vyema mazuri na mabaya yake ukamuachia, wewe angalia maisha yako.
Kama umemuacha, umeamua mwenyewe na huenda kwa kufanya kwako hivyo, unajipeleka kwa mtu sahihi au asiye sahihi. Hukulazimishwa kumuacha, sasa hiyo tangazatangaza ya mabaya yake itakusaidia nini?
Ni kweli leo ndiyo unamuona ana wapenzi wengi wakati mmedumu kwa miaka mingi? Je, ni kweli leo ndiyo unagundua kuwa siyo mjuzi faragha?
Itaendelea wiki ijayo.
Mangapi mazuri ambayo amekufanyia? Mbona huyasemi?
Mimi nadhani tunatakiwa kuacha huu ulimbukeni wa kutangaziana mabaya baada ya kuachana. Hakuna kitu ambacho kinaweza kukufanya ukaonekana wa ajabu kama kumzungumzia vibaya mpenzi wako wa zamani.
Utaonekana unatapatapa kwa kuachwa na wengine watahisi una dhamira ya kumchafulia mwenzako. Matokeo yake sasa wanaume watakuogopa. Hawawezi kuwa na wewe kwa kuwa wanaogopa mkiachana utawatangazia mabaya na udhaifu wao, kitu ambacho si kizuri.
Hivi wewe unadhani huna upungufu ambao mpenzi wako naye akiamua kukutangazia kwa watu utaaibika? Najua kuachwa kunauma sana na wengi wanashindwa kuvumilia ile hali lakini naomba niseme kwamba, ukiachwa shukuru kwani hujui Mungu ana siri gani.
Lakini pia ukipata ujasiri wa kumuacha mtu ambaye ulikuwa unampenda sana, jua kwamba hakukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima ufanye hivyo kisha zilipendwa wako abaki tu kwenye historia kuwa, uliwahi ‘kudate’ na flani.
Kama alikuwa mchovu faragha, alikuwa mchafu, alikuwa kiwembe na mambo mengine, muachie yeye na huyo atakayekuwa naye baada ya wewe.

Note: Only a member of this blog may post a comment.