Katibu wa Uchumi na Fedha Kata
ya Segerea, Steve Massaburi akiwa Hospitali ya Aga-khan leo akiendelea
kuuguza majeraha baada ya kujeruhiwa kwa mapanga nyumbani kwake Segerea
jijini Dar es Salaam jana na watu wasiojulikana.
Steve Massaburi akiendelea kuuguza majeraha, kushoto anayemuhudumia ni jamaa yake Martin Pemba.
Na Dotto Mwaibale
WATU wasiojulikana wamejeruhi kwa mapanga Katibu
wa Uchumi na Fedha Kata ya Segerea Steve Massaburi usiku wa kuamkia juzi
nje ya nyumba yake alipokua akirejea kutoka matembezini.
Kwa mujibu wa Steve aliyelazwa katika Hospitali ya Aga khan, watu
hao wapatao wanne wakiwa na Pikipiki, walimvamia majira ya saa tatu
usiku nje ya geti la nyumba anayoishi na kuanza kumshambulia huku yeye
akijaribu kupambana nao.
Steve ambaye ni mtoto wa Meya wa Jiji la Dar es salaam Dk. Didas
Massaburi, alisema wakati watu hao wakimshambulia walikuwa wakisema wazi
wazi kuwa lengo lao ni kumuona hagombei nafasi ya udiwani katika Kata
hiyo ya Segerea baada ya yeye kuonyesha nia ya kutaka kugombea nafasi
hiyo.
“Walikuwa wakiniambia kuwa wewe si unautaka udiwani sasa utaugombea
ukiwa kitandani au kaburini, hapa hakuna na umaharufu wa mtu kwa kuwa
kila mtu anaitaka nafasi hiyo” alisema Massaburi.
Alisema wakati akiendelea kupambana na watu hao alikuwa akipiga
kelele jambo lililowafanya watu hao kumuacha na kasha kukimbia huku yeye
akiwa amelala chini damu zikimtoka sehemu za shavuni kutokana na panga
alilopigwa.
Pamoja na sehemu ya shavuni, watu hao pia wamemjeruhi sehemu
mbalimbali za mkono wake wa kushoto alipokuwa akijaribu kuzuia panga
kumdhuru sehemu za usoni.
“Kelele nilizopiga ndizo zilizonisaidia kwa kuwa ziliwafanya watu
watoke katika majumba yao kuja kunisaidia wakati huo huo watu hao
wakikimbia kwa kutumia pikipiki zao mbili walizokuwa wamekuja nao”
aliongeza.
Alisema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri tangu alipofikishwa
hospitalini hapo jana huku akishonwa nyuzi zaidi ya ishirini katika taya
lilipigwa na panga na watu hao.
(Na mtandao wa habari za jamii)

Note: Only a member of this blog may post a comment.