Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama
ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na
haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Magomeni Mwanza, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya chama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema:
“Wengi wana hamu ya kutaka kujua mgombea urais wa Chadema, naomba
niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda
hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa
itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM
madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena
tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza
Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi
kadi wanachama wapya waliotoka CCM na kujiunga Chadema, Mbunge wa
Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliweka
msisitizo:
“Muungano wetu wa Ukawa ni wa msingi
sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe wavumilivu, tuache mihemko
ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba
mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM
wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote
mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi
alikuwa ahudhurie mkutano huo lakini kutokana na foleni za Dar es
Salaam alishindwa kuwahi ndege na kwamba, viongozi wengine wa CUF na
NCCR Mageuzi walialikwa lakini walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa ni mpango wa
wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na viongozi wote
wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la Katiba
walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’ wakaondoka
hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.


Note: Only a member of this blog may post a comment.