Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
lipo katika mchakato wa mwisho wa kuanzisha kampuni ya kutengeneza
nguzo za umeme za zege, ikiwa ni mkakati wa uboreshaji huduma kwa wateja
wake, kupunguza matumizi ya nguzo za miti na kudhibiti uharibifu wa
miundombinu hiyo.
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba,
alisema kampuni hiyo ambayo itakuwa chini ya shirika hilo inatarajiwa
kuanza kazi mwishoni mwa mwaka huu mchakato wa kuisajili kwa Wakala wa
Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) utakapo kamilika.
Alisema hatua ya shirika hilo kuanza
kutumia nguzo za zege badala ya za miti ni moja ya mikakati ya shirika
ilo kuhakikisha linatoa huduma bora na za uhakika kwa wateja wake kwani
mara nyingi nguzo za miti zimekuwa hazidumu na kulazimika kubadilishwa
mara kwa mara kutokana na uchakavu.
“Teknolojia
inakuwa kila siku na kurahisisha huduma kwa wananchi na hata wakati
mwingine kupunguza gharama, tutakapoanza kuzalisha nguzo za zege
tutapunguza kero nyingi kwa wateja wetu kwani nguzo za miti huharibika
haraka hasa kipindi cha mvua pamoja nyingine kuungua moto unapotokea,” alisema.
Mramba alisema kutumika kwa nguzo hizo
za zege pia kutabadilisha mandhali ya miji na kuongeza kuongeza fursa za
ajira kwa Watanzania.
Kuhusu uboreshaji wa huduma ya umeme kwa
jiji la Dar es Salaam, Mramba alisema ujenzi wa vituo vidogo vitano vya
usambazaji na upozaji wa umeme unaendelea vizuri pamoja na changamoto
mbalimbali zilizojitokeza katika eneo la Mbagala na Vijibweni na
kusababisha kazi hiyo kuchelewa kukamilika.
Alisema vituo hivyo vilitakiwa kuwa
tayari mwezi ujao lakini kutokana na changamoto hizo sasa vitakamilika
mwishoni mwa mwaka huu na kwamba kituo cha Kinyelezi na City Centre
vinategemewa kukamilika Agosti, mwaka huu.


Note: Only a member of this blog may post a comment.