FILIMBI imeshapulizwa na tayari timu zimeshaanza kuorodhesha wachezaji wake watakaoingia dimbani katika mechi kubwa na ya aina yake hapo Oktoba, kumpata Mtanzania mwingine atakayeingia katika historia ya kuwa wa tano kuliongoza taifa letu.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtangaza John Pombe Magufuli kuwa ndiye atakayepeperusha bendera ya kukitetea huku wenzao kutoka Ukawa wakiwa kimya, wakiendelea na mchakato wa kumpata mtu wao.Lakini michakato ya ndani ya vyama, pia ya kuwapata watu wanaotaka ubunge na udiwani inaendelea. Angalau wabunge kadhaa hadi sasa, Said Arfi (Chadema), Moses Machali (NCCR-Mageuzi), John Shibuda (Chadema), James Lembeli na Ester Bulaya wote kutoka CCM, wametangaza kuhama vyama vyao hivyo.
Kuondoka kwa wabunge hawa kumenipa ufahamu mdogo ambao nimeona siyo jambo baya kama nitawashirikisha mnaofuatilia safu hii ili kuwaweka sawa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, ambao kwa vyovyote vile, utaandika historia ambayo hatukuwahi kuwa nayo kabla.
Nilichojifunza; kamwe usiwaamini wanasiasa. Matatizo yote yanayotokea duniani, ni matokeo ya wanasiasa. Unapoona watu wanaishi kwa amani na wanapata maendeleo, ujue wanasiasa wanahusika, lakini pia unapoona utengano unaoleta uhasama na chuki baina ya jamii, ni matokeo ya wanasiasa wa eneo husika. Matatizo ya wanasiasa ndiyo yanazalisha vita katika Sudan, Libya, Senegal, Iraq, Syria, Palestina na sasa Yemen!
Mwanasiasa ni mtu anayepelekwa na upepo unavyovuma. Matatizo yako siyo kitu cha msingi sana linapokuja suala la masilahi yake kisiasa, kwani yupo tayari kuwaangamiza kwa maelfu ilimradi lengo lake litimie.
Kwao, vifo vya watu ni mitaji, ndiyo maana huwa wagumu sana kuitisha vikao vya kuzuia machafuko, lakini huwa hodari kukaa mezani kujadili namna ya kuyakomesha!
Leo tunashuhudia, waliokuwa wakitukana upande huu, wanakimbilia kulekule na waliokuwa wakikosoa utaratibu huu, leo wanaenda hukohuko. Kwa wasioelewa mchezo huu, wapo njia panda, wanajikuta wamechanganyikiwa wasijue la kufanya. Wanaofahamu vizuri siasa, wanakuambia ni mchezo mchafu kuliko yote unayoifahamu.
Kuna wengine kwa bahati mbaya, tumepandikizwa imani, kwamba chama hiki hasa ndicho chenyewe, au mwanasiasa huyu ndiye anayestahili. Huenda tunaamini hivyo kwa sababu anafanya vile tunavyopenda. Lakini tusichojua, ni kwa nini anafanya tunachopenda!
Hakuna siasa ya kujitolea, yote inakwenda sambamba na masilahi, hasa kwa nchi zinazoongozwa na viongozi wenye ubinafsi kama Afrika. Wakiwa nje ya ulaji, watapiga propaganda ya kuwagombanisha wananchi na watawala, lakini wakipata fursa ya kuishika nafasi hiyo, watafanya yaleyale waliyokuwa wakiyapinga.
Wenyewe wanaoshughulika na siasa wanakuambia hakuna adui wala rafiki wa kudumu. Kwa wewe unayepita mtaani ukitamba na bendera ya chama unachokiamini, lazima ujue maana ya msemo huu. Huenda kwa kutojua kwako, umeshatoa maapizo mengi, umeshacheza kamari kwa kutumia nyumba au mashamba yako na vitu vingine vingi.
Kama wanaohusika wanakuambia adui yako wa leo anaweza kuwa best friend wako kesho, kwa nini wewe ung’ang’ane na uadui au urafiki na mtu kwa sababu ya siasa? Siasa pekee inayoweza kukupa amani, ni ile uliyonayo mwenyewe kichwani mwako.
Itambue hali halisi ya jamii yako halafu waangalie wanasiasa walio mbele yako. Usidanganyike na kelele zao kwa sababu mara nyingi wanazipiga kwa masilahi yao na vyama vyao, wewe ni mtu wa tatu kunufaika na faida wanazotafuta.
Wanasiasa ni binadamu kama sisi, ukimsikiliza utatambua kilichomo ndani ya nafsi yake, ingawa wote wanafanana staili yao ya kutuchota akili. Hata hivyo, angalau wapo ambao maneno yao yanafanana na mahitaji yetu, hao ndiyo tunaowahitaji. Kumbuka, hao ndiyo tunawahitaji, siyo vyama vyao!


Note: Only a member of this blog may post a comment.