Hamida Hassan
Kuna kajitabia kapo kwa baadhi ya mastaa kuficha mimba zao, yaani kuanzia wananasa wanakuwa wasiri hadi siku wanajifungua ndipo utasikia, fulani kajifungua!
Wamefanya hivyo mastaa wengi kama vile Snura Mushi, Jennifer Kyaka na wengineo. Wakati hilo likionekana kuwa la kawaida, sasa tabia nyingine imeibuka ya baadhi ya mastaa kutopenda kuanika sura za watoto wao mara wanapojifungua.
Wenyewe wanadai eti wanaogopa macho ya watu ‘kurogwa’ huku wengine hasa wale waliozaa na wanaume wasiojulikana wakihofia wambeya kuanza kufananisha sura, hicho ndicho wanachokikwepa!
Katika makala haya nitakupa listi ya mastaa waliojifungua siku za hivi karibuni lakini wametumia nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba sura za watoto wao zinabaki kuwa dili.
Zamaradi Mketema
Huyu sasa hivi mwanaye wa pili ana miezi takriban mitatu lakini siyo mimi wala wewe ambao tumewahi kuiona sura ya mtoto huyo.
Mwanaye wa kwanza haikuwa shida, mapema kabisa tulimuona sura yake lakini huyu wa pili imekuwa tofauti. Haijajulikana sababu lakini mwenyewe huenda anataka siku moja atufanyie sapraizi.
Aunt Ezekiel
Alipojifungua ulinzi mkali uliwekwa kuhakikisha hakuna wa kumpiga picha mtoto huyo. Alipobanwa Aunt juu ya mkwara wake huo alidai atamuanika rasmi atakapofikisha siku 40.
Cha ajabu hata siku ya arobaini yenyewe mtoto huyo alifichwa na ikawa ngumu kumpata kiufasaha sura yake kiasi kwamba hata ukiingia kwenye mitandao hutaambulia picha inayoonesha sura ya mtoto huyo aitwaye Cookie.
Marry Mawigi
Huyu aliweka wazi tangu alipojifungua kuwa, mwanaume aliyezaa naye hapendi kabisa mambo ya magazeti wala mitandao. Amepigwa biti kuwa endapo atajisahau akaacha mtoto wake akapigwa picha na zikasambaa kwenye ‘midia’, watagombana na ndiyo sababu ya sura ya mtoto wake huyo kuwa dili.
Hamisa Mobeto
Huyu alificha mimba yake akaja kuanika kitumbo chake akiwa tayari amejifungua, watu wakashangaa sana. Lakini cha ajabu akaendeleza usiri kwa mwanaye ambapo mpaka sasa hakuna aliyefanikiwa kumuona .
Besta Prosper
Ni mke wa mwanamuziki Laurence Malima ‘Marlow’. Huyu naye alijifungua hivi karibuni mtoto wa pili lakini mpaka leo mwanaye hajaanikwa. Hata hivyo, Besta ni kati ya mastaa wenye usiri mkubwa juu ya maisha yake kiasi kwamba si ajabu kumuwekea ngumu mtoto wake.


Note: Only a member of this blog may post a comment.