WIKI iliyopita nilieleza jinsi ya kufanya unapokutana na siku mbaya, ambapo niliweka wazi njia mbalimbali za kitaalam. Nilipata simu na sms nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakieleza jinsi wanavyokutana na nyakati ngumu kutokana na changamoto na matatizo waliyonayo, nimelazimika kutoa somo hili kwa upana zaidi.
Utafiti wa kitaalam unaonesha kuwa, watu wengi sana hawana uwezo wa kustahimili changamoto na matatizo katika maisha. Hufikia hatua ya kujiona kama hawafai na kwamba huo ndiyo mwisho wa maisha yao jambo ambalo kiuhalisia hukosea sana. Kila mtu anapenda kuona maisha yakiwa yamenyooka tu. Kufikia hapo, wanapokutana na tatizo lolote hata kama ni dogo kiasi gani, basi hujikuta wakichanganyikiwa kupita kiasi.Katika kitabu chake cha A Setback Is A Setup for A Comeback, mhamasishaji wa watu kujikomboa na umasikini ambaye pia ni mwanasaikolojia maarufu nchini Marekani, Dk. Willie Jolley aliandika; Problems and challenges are the stepping stones to success (matatizo na changamoto ni ngazi za kupandia kuelekea kwenye mafanikio).
Matatizo na changamoto haziepukiki katika maisha ya binadamu, na hakika hakuna mabadiliko wala kukua endapo hakutakuwa na changamoto na matatizo. Bila matatizo, pasingekuwepo na mabadiliko! Ni lazima kwanza ukutane na maumivu ya matatizo ndipo uweze kukua kifikra na namna ya kutenda mambo maishani.
Mwanasaikolojia maarufu duniani, Johan Wolfgang Van Goeth aliwahi kusema, Problems were designed to make us grow strong (matatizo yaliumbwa kutufanya tuwe imara). Ni lazima mtu aumie mara nyingi ndipo mafanikio ya kweli yaje.
Tofauti ya shuleni na katika maisha ya kawaida ni kwamba, shuleni tunapata kwanza somo ndipo tunapewa testi, lakini katika maisha tunapata kwanza testi ndipo tunajifunza somo! Kamwe usiyatazame matatizo na changamoto kama mwisho wa kila kitu maishani mwako, bali yatazame matatizo kama njia ya kuelekea kwenye ushindi wako.
Cha muhimu ni kuwa na ndoto kubwa za kufikia na kujiwekea malengo madhubuti ya namna ya kufanikisha ndoto zako. Hata hao unaowaona kuwa ni matajiri wakubwa, walikutana na matatizo makubwa mno pengine ukiyasikia unaweza usiamini kwa urahisi, pia hata sasa hivi bado wanakabiliana na changamoto nyingi.
Usijaribu kuhamaki kila unapokutana na matatizo na changamoto, jikite sana kwenye kutafuta suluhu ya matatizo hayo, yaone kama njia muhimu ya kukufikisha huko uendako maishani mwako.
Maisha bila changamoto na matatizo hayana maana tena, ni lazima kuwepo na changamoto ndipo akili zako zipate mwanya wa kujichanganua na kupata suluhisho halisi. Hata mtoto anapokuwa anajifunza kutembea, huanguka mara nyingi mno na wakati mwingine hupata majeraha makubwa lakini hizo ndizo huwa hatua muhimu za kukomaa na hatimaye kujikuta akitembea.
Matatizo ni muhimu sana katika kila hatua ya mafanikio maishani. Hakikisha unajifunza somo kubwa katika kila tatizo unalokutana nalo na kila siku endelea kumuomba Mungu akuwezeshe kupata unachokitaka huku ukiongeza juhudi na bidii katika kufanya kazi zako, kwani hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati mbaya au kwa njia ya miujiza, ni lazima mtu upambane kwa kumaanisha huku ukikabiliana na kila changamoto inayojitokeza mbele ya safari yako ya kuelekea kwenye ushindi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.