JOTO la Uchaguzi Mkuu linazidi kupanda miongoni mwa wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa, huku idadi kubwa ya wasanii wakionesha nia ya kutaka kuitwa waheshimiwa kuanzia mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
Hadi sasa baadhi ya waliotangaza nia ni Joseph Haule (Profesa Jay), Zuwena Mohamed (Shilole), Wema Sepetu, Steve Mengere ‘Steve Nyerere’, Jacob Stephen (JB), Mrisho Mpoto na wengineo kadhaa, wakitaka kwenda kuungana na wenzao Joseph Mbilinyi wa Chadema pamoja na Vicky Kamata kutoka CCM.
Hakuna mwenye uhakika nini hasa kitatokea katika uchaguzi huo, ingawa uwezekano wa wasanii hao kuleta ushindani na hatimaye kushinda ni mkubwa, hasa ukirejea jinsi Sugu alivyoingia pasipo kutarajiwa na wengi. Ingawa waigizaji hawa wamekuwa na mambo kadhaa nje ya uwanja, hilo haliwezi kuwa jambo lenye kutia shaka juu ya uwezekano wao wa kushinda.
Wengi wamekuwa wakipiga picha na kuona taswira ya bunge hilo litakalokuwa na wasanii hawa, kwani huenda likaongeza mvuto na kulifanya kuwa moja kati ya mabunge yatakayotazamwa sana na watu, kwa lengo la kuwasikia tu wanachosema, bila kujali kama kitakuwa cha maana au lah.
Kwa ambao wamekuwa wakifuatilia vikao vingi vya Bunge katika miaka ya karibuni, wameliona kama lililopoteza mwelekeo ambalo linatumia muda mwingi kwa wabunge kurushiana vijembe bila kujali kama mada iliyo mbele yao ina masilahi gani kwa taifa lao.
Wengi wamekuwa wakikerwa na jinsi wabunge wengine wanavyopoteza muda kuzungumza mambo yasiyo na tija kwa taifa na badala yake kuweka mbele sana itikadi ya vyama vyao, hata kama kinachojadiliwa mbele yao ni kitu muhimu kiasi gani kwa nchi yao.
Kwa staili hiyo ya ubunge, wasanii hawa wana nafasi kubwa ya kushinda kupitia vyama vyao, kwani watu wanaona ni bora kuwaona waigizaji orijino wakiigiza bungeni, kuliko wabunge ambao mara nyingi wanaonekana kuwa wasio na mchango mkubwa kwa taifa.
Hata hivyo, hivi ni kweli wasanii hao wamejipima na kujiona wanatosha kuwania ubunge au ni ile janja ya siku hizi ya kutangaza nia ili kuwatia hofu wengine wanaotaka nafasi hiyo?
Maana taarifa ambazo siyo rasmi, zinasema siku hizi watu wengi hutangaza nia makusudi ili kuwapa presha wabunge kwenye majimbo yao, wakiamini kuwa baadaye watafuatwa na ‘kupozwa’ kitu kidogo, kama ambavyo uvumi huo umewahi kuhusishwa na watu kadhaa hapo nyuma.
Kwa sababu katika hali ya kawaida, ni kwa namna gani baadhi ya wasanii hawa, ambao maisha yao yamejaa utata wataweza kupewa kura na wananchi wanaohitaji watu makini wenye kujua matatizo na suluhisho lake?
Siwadharau, lakini siyo vibaya kuwakumbusha kuwa ubunge siyo kitu rahisi kama kupata uongozi wa Bongo Movie au kuwa muigizaji mkuu katika filamu. Ni zaidi ya kuwaimbisha watu katika majukwaa ya muziki yaliyojaa vijana wengi.
Wanapaswa kujua, ubunge unahitaji mtu mwenye uwezo wa kujenga hoja na anayejua wananchi wanahitaji na si vinginevyo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.