Wednesday, June 17, 2015

Anonymous

KUMEKUCHA YANGA SC! Nakwenda kumleta mrithi wa Msuva -Pluijm Ajigamba!

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Mohammed Mdose,Dar es Salaam
KUFUATIA mkataba wa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva kubakia mwaka mmoja huku akionyesha hana nia ya kutaka kuendelea kukaa kwenye klabu hiyo, kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, amesema hatapenda kuona uongozi wa Yanga ukimlazimisha kiungo huyo kusaini mkataba mpya.

Pluijm amesema kama mchezaji huyo atataka kuondoka, haoni haja ya uongozi wa Yanga kumbembeleza na ikiwezekana atakwenda nchi za Ghana, Senegal na Cameroon kutafuta mbadala wake.

Mwezi uliopita, Msuva alikwenda nchini Afrika Kusini kufanya majaribio kwenye timu ya Bidvest Wits, inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo (PSL), lakini mpaka sasa majibu hayajawekwa wazi kama amefuzu au la.

Akizungumza na Championi Jumatano, Mholanzi huyo ambaye hivi karibuni aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2014/15, ikiwa ni mara ya 25, alisema anautambua mchango mkubwa wa kiungo huyo ndani ya Yanga, lakini kama atataka kuondoka na aende kwani anaamini atampata mbadala wake mara moja.

Alisema kuwa wakati yupo mapumzikoni nyumbani kwake nchini Ghana, alipata taarifa za kutaka kuondoka kwa kiungo huyo ambaye ameibuka kuwa mfungaji na mchezaji bora msimu huu, lakini hazimuumizi kichwa kwani anaamini watakaobaki wataifanya Yanga iendelee na makali yake yaleyale.

“Msuva alifanya kazi nzuri msimu ulioisha hivi karibuni lakini siwezi kutumia nguvu nyingi kumlazimisha asiondoke.
“Unajua kama mchezaji anataka kuondoka unamwacha, akiondoka nitafunga safari hadi Afrika Magharibi kumfuata mbadala wake, naamini nitampata tu bila wasiwasi,” alisema Pluijm.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.