BAADA ya kumrudisha mshambuliaji wake Paul Kiongera, uongozi wa Simba umepanga kumfanyia vipimo mchezaji huyo kuona kama yupo fiti.
Kiongera alitua Simba msimu uliopita ambapo alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili ambao alishindwa kumaliza msimu uliopita kufuatia kujitonesha goti lake la kulia katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union na kupelekwa nchini India kufanyiwa upasuaji na baadaye kupelekwa kwa mkopo katika timu ya KCD ya Kenya.
Kikizungumza na Championi Jumatano, chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeeleza kuwa licha ya uongozi kuamua kumrejesha mchezaji huyo, lakini wanahitaji kumfanyia uchunguzi ili kumuona kama yupo fiti.Aidha, chanzo hicho kilieleza kuwa, mchezaji mwingine ambaye anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina kabla ligi haijaanza ni Samir Haji Nuhu ambaye alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu kwa muda mrefu.
“Uongozi wa Simba bado unaendelea kusajili wachezaji kwa ajili ya kukiimarisha kikosi ili kisiweze kuyumba kama ilivyokuwa msimu uliopita.
“Kiongera ni miongoni mwa wachezaji walioongezewa nguvu lakini kabla hajaanza kutumika, uongozi umepanga kumfanyia ‘check up’ ya nguvu kuweza kuangalia tatizo lake lililokuwa likimkabili kama yupo fiti ili kumtumia lakini mchezaji mwingine anayetaka kufanyiwa vipimo ni Nuhu aliyetokea Azam FC,” kilisema chanzo hicho.

Note: Only a member of this blog may post a comment.