Wednesday, May 27, 2015

Anonymous

YANGA noma sana! Yanasa wengine wawili!


Beki wa kushoto kutoka KMKM, Haji Mwinyi, aliyesajiliwa na Yanga.
Hans Mloli,Dar es Salaam
YANGA noma sana! Imedhihirisha kwamba ipo ‘serious’ na haitaki masihara baada ya jana kumalizana na majembe mawili mapya zikiwa zimepita siku mbili pekee tangu imsajili kwa kishindo kiungo machachari, Deus Kaseke kutoka Mbeya City.

Wachezaji hao waliomwaga wino huo ni pamoja na beki wa kushoto kutoka KMKM, Haji Mwinyi aliyepewa kandarasi ya miaka miwili kwa kitita cha Sh. Mil 20 na kipa wa Kagera Sugar, Benedict Tinoco aliyesaini mkataba wa miaka mitatu.
Taarifa zinaeleza kuwa, Mwinyi alikuwa Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizana na Yanga ambapo mapema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo lililofanyika makao makuu ya timu hiyo yaliyopo Mtaa wa Jangwani, Kariakoo jijini Dar, alielekea bandarini kuchukua boti na kurejea kwao Zanzibar.

Pamoja na hayo, mchezaji huyo pia ameahidiwa kutekelezewa mambo mengi na vigogo hao wakati akiwa Dar akiichezea timu hiyo ikiwa ni pamoja na kupewa nyumba yenye hadhi ya juu huku masuala ya usafiri yakibaki kuwa majaliwa ya hapo baadaye.

Championi Jumatano limezungumza na Mwinyi na akatamka machache kuhusiana na usajili wake huo huku akiwaahidi Wanajangwani mambo mazuri msimu ujao.

“Nimemalizana na Yanga leo kwa kusaini miaka miwili, naamini nakuja kuitumikia timu nzuri na nitajitahidi kufanya vizuri msimu ujao kwa ajili ya timu nikishirikiana na wenzangu, kwa sasa naelekea nyumbani kwanza kisha nitarudi huku Dar kwa ajili ya timu ya taifa, tumekubaliana mambo mengi na Yanga lakini yanabaki kuwa siri ya mkataba,” alisema Mwinyi.
Kwa upande wa Tinoco, Yanga wanaonekana kulamba dume kutokana na uwezo wa kipa huyo ambaye alikuwa kipa bora wa michuano ya Copa Cocacola.

Hata hivyo, kipa huyo anaonekana kuwa na uzoefu wa kutosha kwa kuwa amedumu kwa muda mrefu sana kwenye kikosi cha Taifa Stars Maboresho ambacho kipo chini ya kocha Mart Nooij.Usajili wa kipa huyu unamaanisha kuwa safari ya Alphonce Matogo ambaye alikuwa kipa namba tatu wa Yanga imewadia.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.