KAMA imejibu mapigo kwa Yanga ambayo ilimsainisha Deus Kaseke kutoka Mbeya City, Simba inatumia Sh Milioni 40 kumshawishi straika wa Mgambo JKT, Malimi Busungu ajiunge nao.
Katika ishu ya Kaseke, Simba ilikuwa imeshamalizana na winga huyo wakati wa usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana, Yanga ikaingilia kati lakini mambo yakagoma kwani mchezaji alikuwa na mkataba bado lakini mwanzoni tu mwa usajili huu, Yanga wakapiga bao.
Sasa katika ishu ya Busungu anayesifika kwa kuzifumania nyavu, Yanga ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumwania straika huyo na kuzungumza mambo kibao ya maslahi.Hata hivyo, Simba baada ya kupigwa bao katika usajili wa Kaseke, ikasema liwale na liwe, lazima Busungu anasaini kwao na hadi jana mchana ilikuwa imekubaliana naye ajiunge nao kwa dau la Sh Milioni 40.
Akizungumza na Championi Jumatano, Busungu alisema kuwa ametua ndani ya klabu hiyo baada ya kufanikiwa kumalizana na viongozi wake kwa kumpatia mahitaji aliyotaka na kuachana na Yanga.
“Najiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili na wakati wowote watanipa dau la Sh Milioni 40, nimekubali na kuzipiga chini ofa zote ikiwemo ile ya Yanga,” alisema Busungu aliyefunga mabao tisa katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Kama Simba ikifanikiwa kumsajili Busungu itakuwa imesajili mchezaji wa pili ndani ya siku chache kwani Jumapili iliyopita ilimsajili Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City.
Note: Only a member of this blog may post a comment.