Tuesday, May 26, 2015

Anonymous

Usajili SIMBA SC, YANGA SC ni VITA!


Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji.
Wilbert Moland na Sweetbert Lukonge
KWELI Yanga na Simba wamepania kuimarisha vikosi vyao, ila hali ilivyo sasa utafikiri ni vita.
Maana kila upande haulali na unataka kuhakikisha unapata wachezaji bora ila usiku wa kuamkia jana ilikuwa kama filamu wakati Yanga na Simba zilipogongana kwa wachezaji Deus Kaseke na Peter Mwalyanzi.
 

Yanga ilituma tiketi ya ndege kwa Kaseke lakini wakati anatua Dar es Salaam, Simba walikuwa wanajiandaa kumpokea, lakini wakakwama baada ya kuambiwa anatua Dar es Salaam saa 1:30 usiku.Kumbe Kaseke alitua Saa 12:45 jioni na kupokewa na Yanga ambao walifanya naye mazungumzo, wakamalizana kabla ya Simba nao kumfuata usiku hadi saa 7 usiku walikuwa naye, ikashindikana, Yanga wakamsajili. 

Simba walipata dalili za kushindwa mapema, wakaelezwa kuwa Mwalyanzi naye alikuwa akiwaniwa na Yanga, hali iliyowafanya waone watawakosa wote, haraka wakatuma tiketi Mbeya, jana asubuhi akawasili.

Mara baada ya kuwasili, haraka alipokewa na Collins Frisch ambaye aliungana na Kassim Dewji kuhakikisha wanacheza ‘mchezo salama’ kabla ya kufika kwa Mwenyekiti wa Usajili, Zacharia Hans Poppe ambaye aliungana nao kufanikisha usajili huo.
Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe.
Wakati Mwalyanzi akiwasili uwanjani hapo, naye alikuwa akisubiriwa na Yanga, ndipo Simba wakalazimika kumpitishia mlango mwingine wa VIP.Taarifa zinaeleza Yanga imemwaga Sh milioni 35 kwa Kaseke na mshahara wa Sh milioni 2 na ahadi ya nyumba ya kuishi wakati wote atakaokuwa Dar akitumika, wakati Simba imempa Mwalyanzi Sh milioni 20 na mshahara wa Sh 800,000 kwa mwezi. 

Kila mmoja kasaini miaka miwili.  “Kwa sasa Mwalyanzi ni mchezaji wetu, tumeingia naye mkataba wa miaka miwili. Tulikuwa tukiwasiliana naye na leo (jana) tumefanikiwa kumalizana, hatuwezi kusema kwa sasa kwamba nani anafuata lakini tunaendelea kufanya mazungumzo, mambo yakikamilika tutaweka wazi,” alisema Hans Poppe. 

Bado Simba inaonekana kuhaha kusaini mkataba mpya na Said Ndemla ambaye bado ana mwaka mmoja huku ikiwa imeongeza mkataba wa Hassan Isihaka na William Lucian Gallas pia juhudi zinafanyika kumnasa straika Mrundi, Laudit Mavugo. 

Yanga imeshaongeza mkataba mpya na Haruna Niyonzima (miaka miwili) na Mbuyu Twite (mmoja) huku wakiendelea kumsubiri Kocha Hans van Der Pluijm ambaye anatakiwa kutua na vifaa viwili au vitatu.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.