MIRIAM Jolwa siyo jina geni miongoni mwa mashabiki wa filamu za Kibongo. Ni mmoja wa mabinti walio wadau katika tasnia hiyo, ingawa amekuwa maarufu zaidi kwa jina lake la kisanii kama Jini Kabula.
Nina uzoefu kidogo na wasanii wetu, hasa hawa wakubwa. Baadhi yao nimewafahamu tangu wakiwa hawana umaarufu hadi kufikia ustaa wa kutisha. Majina yao yanapopaa na kuwa gumzo kila kona, dunia inakuwa yao, ndiyo maana wapo ambao wanashindwa kupanda daladala, wakiamini kuna watu watawashangaa.
Wanaamini ukubwa wa majina yao unawafanya waonekane tofauti na binadamu wengine, wakidhani wakionekana wamepanda usafiri wa umma, tafsiri ya watu itakuwa wamefulia, au hawana kitu. Juzikati kuna staa mmoja mkubwa alitutembelea ofisini kwetu, kuna wenzangu wanamfahamu, mimi sikuwahi kumuona zaidi ya kusikia jina lake.
Nilipouliza huyu ni nani, wenzangu walinishangaa wakiniuliza inakuwaje simfahamu huyo supastaa. Wao walinishangaza zaidi. Nikiamini kwamba suala lile dogo litakuwa limeishia pale, nikaja kushangaa zaidi baadaye nilipoambiwa kuwa supastaa yule alipiga simu kwa marafiki zake ofisini kwetu, akisema siku hiyo alikuwa amedhalilishwa sana, kisa eti mimi kutomfahamu!
Na hili ndilo tatizo la karibu wasanii wote waliobahatika kukuza majina yao. Wanaamini kila mtu anawajua, bila kufahamu kwamba kuna mtu Bongo hiihii, hajawahi kusikiliza Bongo Fleva, hajawahi ona Bongo Movie na wala hasomi magazeti ya burudani. Lakini hata kama wanaona, wanasikiliza na kusoma magazeti pendwa, bado hawashoboki nao.
Kwao, kupishana na watu kumi bila mtu kuwashangaa, ni tatizo. Kama siyo kufikiri wanarogwa, basi wanaamini watu wamewasahau. Ili kurejesha utambuzi wao, baadhi yao hufanya vituko ambavyo wenyewe wasanii wanaita kiki. Ndivyo alivyofanya Jina Kabula, ambaye jina lake ni kama linalofifia kwenye ‘media’.
Jini Kabula alipiga picha zikionyesha mwili wake ukiwa mtupu, huku mikono yake ikitumika kuziba matiti yake na sehemu zake nyeti. Zimesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii. Katika utetezi wake, anasema rafiki yake wa kiume ndiye aliyempiga picha hizo na kuzisambaza, baada ya kutokea tofauti baina yao.
Ni utetezi dhaifu usio na mashiko, kwa sababu ukizitazama picha hizo, unajua kabisa ni za mtu aliyejiweka tayari kwa kupigwa, au kama wenyewe wanavyosema kuwa alikuwa ameweka pozi!Ni wazi, anataka watu wainue vichwa vyao kumtazama. Ni kweli, kwa picha hiyo, anatazamika. Lakini kwa watu wenye macho ya udadisi, wanamuona kwa namna ambayo haivutii, ni kama wanamuona mtu anayejinadi, akitaka watu wauone mwili wake ili wahamasike.
Sijui wengine wanafikiriaje, lakini binafsi naona kama mwanamke mtulivu, asiye na makeke, mwenye kuona aibu na mwili wake ndiye mzuri na ambaye wanaume wanamhitaji?
Inawezekana picha imevuja kwa bahati mbaya, lakini tathmini binafsi ya mtu ni kitu muhimu sana katika kuchuja na kupima njia tunayopita. Ni kweli, fanya kile akili yako inapenda, lakini katika maisha ya ustaa tunaousaka, baadhi ya mambo tunalazimika kuishi kama vile jamii inavyotaka, vinginevyo tutaishia kuwa vichekesho!

Note: Only a member of this blog may post a comment.