Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe,
ameeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuwapatia kazi ya ujenzi wa
Bandari ya Mwambani mkoani Tanga watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Amesema watuhumiwa hao wamepewa kazi hiyo kupitia Mradi wa Mwambani Economic Corridor (MWAPORC), ambao utagharimu Sh trilioni 54, huku kukiwa hakuna taratibu za utangazaji wa zabuni zilizofuatwa na Serikali.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa
akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika miji ya Mafinga na
Iringa mkoani hapa ambapo alisema Serikali imeipa kazi ya ujenzi Kampuni
ya VIP Engineering and Management inayomilikiwa na James Rugemalira
ambaye anahusika katika sakata la Escrow.
Zitto alisema ACT-Wazalendo wanamtaka
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta afanye uchunguzi kuhusu mradi huo wa
Mwambani na achukue hatua kwa kile alichodai kuwa utapeli wa watu wa
Escrow.
“Taratibu hazijafuatwa, hakuna zabuni iliyotangazwa kuhusu Bandari ya
Mwambani, miradi mikubwa kama hii Serikali hutakiwa kutoa ‘guarantee’
kwa mikopo ambayo inachukuliwa.
“Hivyo kuhusika kwa Rugemalira wa Escrow na mwanasheria Cathbert Tenga
wa Richmond kwenye mradi huu ni mwendelezo wa miradi ya kitapeli,” Zitto.
Zitto ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema uzito wa mradi huo wa bandari unakwenda sambamba na reli ambayo itafika hadi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Akitoa taarifa kuhusu mradi huo hivi karibuni, msimamizi wa mradi huo ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini, Cathbert Tenga, alisema utamilikiwa na Watanzania wenyewe na si watu kutoka nje ya nchi kama ilivyo katika miradi mingine.


Note: Only a member of this blog may post a comment.