Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete
kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na
kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye
anawatuma.
Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa
hilo jana, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya
Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.
“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa… asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.
Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao
walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo
kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10
yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.
“Mimi
ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si
Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,”.
“Madaktari,
wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini
hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila
mtakapopotoka, nafanya kazi ya bwana,” .
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na
vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza
idadi gani ya waumini.
Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.
“Waumini
hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu
nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?”
alisema na kisha kuwauliza waumini hao… “Hivi baba yenu nikiwaomba kila
mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”
-MWANANCHI

Note: Only a member of this blog may post a comment.