Martha Mboma, Dar es Salaam
BAADA ya mshambuliaji Mtanzania
wa TP Mazembe, Mbwana Samatta kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa
Afrika na timu yake kutwaa ubingwa, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, amefunguka kuwa straika huyo anatakiwa kucheza kwa kujiamini kuhakikisha anaibeba Stars dhidi ya Algeria Jumamosi.
Kerr alisema kuwa Samatta ni mmoja wa
wachezaji wenye vipaji na uwezo wa kufanya vizuri zaidi na amefanikiwa
kumshuhudia akiitumikia timu ya taifa hapa nchini, hivyo akishirikiana
vyema na wenzake, anaweza kuifikisha mbali Stars.
Akizungumza akiwa Afrika Kusini, kocha
huyo alisema mshambuliaji huyo anatakiwa kujituma kwa bidii
akishirikiana na wenzake ili kuweza kuandika historia nzuri zaidi kwa
Waarabu hao.
“Samatta nimeona uwezo wake kupitia
mechi za timu ya taifa ya hapa Tanzania lakini ni mmoja ya wenye vipaji
ambao nchi hii inatakiwa kujivunia pia kutokana na kufanya vyema akiwa
na klabu yake ya TP Mazembe, sasa ni wakati wa kuonyesha kweli anaweza
kwa kuiongoza Stars dhidi ya Algeria akishirikiana na wenzake.
“Cha msingi anatakiwa kujiamini na
ajitume uwanjani, atafanikiwa na kuweza kufika mbali zaidi ya hapo alipo
sasa, hasa kipindi hiki ambacho ana jukumu zito kuisaidia timu yake ya
taifa,” alisema Kerr.

Note: Only a member of this blog may post a comment.