Badala yake imewatupia lawama wakuu wa shule zilizoamua kuwarudisha wanafunzi makwao kutokana na kukosa chakula cha kuwalisha.
Baadhi ya shule za sekondari nchini hivi karibuni zilifungwa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula baada ya wazabuni kugoma kuwasambazia chakula kwa sababu hawajalipwa fedha zao kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumannne Sagini alisema mkuu wa shule mwenye mamlaka ya kufunga shule hizo ni Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Alisema Serikali hutoa huduma ya chakula kwa shule za sekondari za bweni na shule za msingi elimu maalum za bweni kwa kuzingatia fedha zilizotengwa na upatikanaji wake katika mwaka husika.
Alisema fedha za chakula hutolewa kwa awamu na kukamilishwa katika kipindi cha mwaka wa fedha unaotekelezwa.
“Kati ya Julai 2014 hadi Machi 2015, Serikali imetoa Sh bilioni 28.1 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi ambazo ni sawa na asilimia 66.7 ya Sh bilioni 42.1 zilizotengwa kwa mwaka 2014/15. Kiasi kilichobaki ni Sh bilioni 13.9 sawa na asilimia 33.23 ya fedha zilizotengwa,”alisema.
Sagini alisema kiasi hicho cha fedha hupelekwa katika hamashauri na baadaye wazabuni hulipwa kwa kuzingatia huduma waliyotoa kwa kila shule.
“Shule nyingi zilikuwa katika kipindi cha mapumziko mafupi kati ya Machi 28, hadi Aprili 14, mwaka huu… katika kipindi hiki wanafunzi walitakiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya mapumziko na shule nyingi zimefungua April 8, mwaka huu na nyingine April 12, hivyo wanafunzi walikuwa nyumbani katika mapumziko mafupi ya kawaida,” alisema.
Hata hivyo alisema walipokea taarifa kwamba baadhi ya wakuu wa shule zikiwamo za Rugambwa, Kahororo, Nyakato, Ihunga (Kagera), Lyamungo (Kilimanjaro), Mpwapwa, Abeid Aman Karume (Dodoma), Kazima, Milambo, Tabora wasichana na wavulana walisogeza mbele tarehe za kufungua shule baada ya mapumziko mafupi kwa madai kuwa hawakuwa na fedha za chakula.
“Kwa kifupi ni kwamba Serikali haijafunga shule na wakuu wa shule waliotangaza kufunga shule hizo chache wamefanya makosa kwa kuwa hawakuwasiliana na mamlaka zinazohusika kupata kibali kama kuna sababu ya kufanya hivyo,” alisema Sagini.

Note: Only a member of this blog may post a comment.