Picha sio ya tukio halisi!
Wakazi wa Kibamba nje kidogo ya jiji la
Dar es salaam jana walifurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph kushuhudia
maajabu ya tukio la kufufuka kwa mtoto anayedaiwa kufariki dunia mwezi
Agosti mwaka jana.
Mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja
inadaiwa alizikwa katika makaburi ya Mlongazila na alifariki Agosti 7
baada ya kuugua gafla na kuishiwa damu.
Mtoto huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai
na Juma Nakochinya (33) maarufu kwa jina la Bino, mkazi wa eneo la
Pandambili mkoani Dodoma ambaye hutibu kwa njia ya maombi.
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Hellena Mtoro,
alisema ilikuwa siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo
mwanawe akiwa na umri wa miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza
hospitali ya Mbezi kwa matibabu.
Alisema baada ya kufika hospitalini
hapo, vipimo vilionyesha ameishiwa damu hivyo alihamishiwa hospitali ya
Tumbi, iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
“Madaktari
walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta mishipa ya damu maeneo
tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa ilikuwa ikionekana
lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika, ilipofika saa
6:00 usiku alifariki dunia,” Mtoro,
Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.
“Ukweli
ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha kawaida, hivyo tulianza
maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora Peter, ambaye
baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye maombi na
kututaka tumpelekee picha yake,”
“Baada
ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo hai na anaamini
atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja nilikutana na mama
Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu, aliniambia
kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa
kichawi,”
Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.
“Nilifanya
hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado hewani, alinijulisha kuwa
mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende kesho yake Dodoma
kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,”
Hellena alisema siku iliyofuata
alisafiri kuelekea Dodoma na aliwasili saa 10:00 jioni ambapo alienda
moja kwa moja kwa mganga huyo.
“Saa 1:00 jioni Bino alichukua mwiko,
ungo na kinu, vifaa anavyovitumia kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini
na akaanza kusoma dua kisha nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule,
nilishtuka sana baada ya kumwona akiwa hana hata nguo, amechafuka na
aliyechoka,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.
“Jana aliletwa na Bino ili aje
kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa sababu hali ya mwanangu
inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ” alisema.
Baba wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa
tukio hilo ni la kwanza na la aina yake kwenye ukoo wao na kwamba
lilipotokea hakuna aliyeamini hadi walipomuona mtoto.
Alisema baada ya mtoto wake kuletwa,
majirani ambao walishiriki kwenye msiba wake, walishtuka na kujaa
nyumbani kwake kitendo ambacho kiliwalazimu kwenda polisi kutoa taarifa
ya kile kilichotokea.
-NIPASHE


Note: Only a member of this blog may post a comment.