Baadhi ya waigizaji wa filamu nao hawajalaza damu, wametangaza nia yao ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, macho yao yakielekezwa kwenye Ubunge.
Dude, Tabora Mjini
Ni msanii wa maigizo anayegombea ubunge katika jimbo la Tabora Mjini. Dude alisema; “Nimeanza kufanya maandalizi ya kugombea ubunge nyumbani kwetu Tabora mjini, niko tayari kuchuana na yeyote na sasa niko kwenye maandalizi ikiwemo kuwa karibu na wananchi kwani wananikubali, hivyo nitahakikisha ninapata ushindi.” Mbunge wa sasa ni Ismail Aden Rage ameshatangaza kwamba hatagombea tena.
JB, Kinondoni
Muigizaji maarufu kwa jina la Bonge la Bwana, amesema yupo mguu sawa kuingia kwenye ulingo wa siasa kwa kugombea ubunge mwaka 2015. JB anasema,“Nitajitosa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha ubunge. Nia ninayo, uwezo ninao na sababu pia ninayo, ni muda mwafaka sasa wa kutimiza ndoto yangu ya kuitumikia jamii.”
Hata hivyo, JB hajaweka wazi jimbo gani atagombea lakini anatajwa kugombea ubunge kwenye jimbo la Kinondoni ambalo kwa sasa liko chini ya Idd Azzan- CCM.
Steve Nyerere, Kinondoni
Mwigizaji huyu alipata umaarufu zaidi kwa kuigiza sauti ya mwalimu Nyerere, Steve Nyerere ametangaza nia ya kugombea ubunge mwaka huu kwenye uchaguzi mkuu katika Jimbo la Kinondoni. Amejipanga kuwania kiti hicho kwa tiketi ya CCM.
Nyerere anasema, “Ukiona chereko chereko ujue mambo yameiva, nitagombea ubunge 2015. Nimejipanga na ninaweza kufanya hivyo, nipo vizuri sana.” Jimbo hilo la Kinondoni liko chini ya Mhe. Idd Azzan (CCM)
Dokii, Kilosa Morogoro
Dokii anayo nia ya kugombea ubunge mwaka huu kwenye jimbo la Kilosa Morogoro. Anasema, “Nitagombea ubunge katika jimbo la Kilosa, naomba tu Neema ya Mungu iniongoze kwa sababu kila kitu huwa nafanya na kusikiliza nini Mungu anaongea na mimi, nia yangu ni kugombea Kilosa sababu ndipo nilipotokea huko kwani nimekulia Kilosa Kimamba Morogoro.”
Anasema, “Mimi ni msanii pekee naweza kusema ndiyo nimetumika sana kwenye jamii kuliko wasanii wote, kwenye kuelimisha jamii najitolea hata kipindi kile cha madereva wa bodaboda mpaka wakanipa Ubalozi nilikua natetea haki zao, pia nataka kuonyesha kwamba wanawake tunaweza.”
Jimbo la Kilosa liko chini ya Mustafa Mkulo (CCM) ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha kabla ya kujiuzulu. Mbunge huyo ameweka bayana kwamba hatagombea katika uchaguzi wa 2015.
King Majuto, Tanga Mjini
Mchekeshaji King Majuto ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tanga Mjini, katika uchaguzi wa mwaka huu ambapo kwa mujibu wa maneno yake anasema lengo kubwa ni kutaka kuinua uchumi wa Tanga pamoja na kutetea haki za wananchi pamoja na rasilimali za Mkoa huo. “Nitarudisha Tanga ya zamani ambayo ilikuwa ikisifika sehemu mbalimbali kutokana na rasilimali zilizopo ambazo kwa sasa zimeshindwa kusimamiwa na kuwanufaisha watu wa Tanga,” alisema Majuto ambaye atakua akichuana na mbunge wa sasa wa Tanga Mjini, Omari Nundu (CCM).
Shilole, Igunga
Shilole si mgeni katika kuota vitu vikubwa. Shilole amepanga kugombea ubunge kwenye jimbo analotokea la Igunga mkoani Tabora katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Shilole amesema anamanisha na nia hiyo na kama Mungu akipenda atakuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Baada ya Dalali Kafumu anayefuata ni mimi, mimi nadhani napenda jimbo langu na nawapenda wakazi wangu wa Igunga wananiona tangu nakua mpaka sasa hivi, kwa hiyo wanafurahi. Sasa wananiambia ‘sisi hatutaki kumpa mtu mwingine kiti hiki sasa na hivyo wananipa changamoto,” alisema msanii huyo.
“Vitu viwili vya kwanza ambavyo nitavifanya nikiingia kwenye lile bunge nikiwa kama msanii, kwanza nitatetea haki za wasanii, cha pili Igunga yangu wapo wakazi wa Igunga vijana wapate kazi, yaani akinamama, wale mama lishe na wengine lazima wawe na kazi zao. Kwahiyo nitawatafutia kazi na nitajenga chuo cha muziki,” alijinadi msanii huyo.
Kingwendu
Mwigizaji Kingwendu, anasema anajiandaa kugombea ubunge mwaka huu 2015.Hata hivyo, Kingwendu hakuweka bayana atagombea jimbo gani wala kupitia chama gani, isipokuwa zaidi anasema kuwa chama ambacho kinapendwa na Watanzania wengi ndicho atatumia tiketi yake.
Kingwendu anasema, “Ninajiandaa kugombea ubunge 2015 kupitia chama ninachoona kinapendwa na Watanzania wengi kwenye jimbo ambalo nitalitaja hapo baadaye wakati utakapofika, bado ninafanya mazungumzo na washauri wangu wa karibu kuhusiana na suala hilo, nadhani nitaliweka wazi muda ukifika.”
Chanzo: Mwanaspoti

Note: Only a member of this blog may post a comment.