Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila
baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua
ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili
walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata
hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa
mkutano wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni, liliibuliwa na
Gazeti la The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi
Communications Ltd na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili
kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia
zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za binadamu nchini.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo
vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na
hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa
zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za
binadamu kwa mwaka jana.
-MWANANCHI


Note: Only a member of this blog may post a comment.