Ofisi za jengo la tawi la Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo
la Dimani, mkoa wa Mjini Magharibi, limeteketea kwa moto na kusababisha
hasara kubwa ya vitu vilivyokuwamo humo ingawa thamani ya vitu hivyo
haijajulikana.
Tukio hilo lilitokea mtaa wa Kisauni usiku wa kuamkia jana saa nane usiku.
Mashuhuda walisema watu wasiojulikana
walifika na gari aina ya Pick-up na kuvunja mlango wa ofisi hizo na
kulilipua jengo hilo kwa petroli.
“Majira
ya saa nane usiku ilikuja gari na watu wawili walishuka katika gari
hiyo na kuingia ndani huku wakisikika wakisema tayari tuondoke na baada
ya kuondoka tu jengo hilo lililipuka,” alisema shuhuda mmoja aliyekuwapo katika eneo hilo.
Alisema baada ya kuona moto na moshi mkubwa ukiwa umetanda ndipo walipowapigia watu wa Zima Moto na walifika kuuzima.
Diwani wa wadi ya Tomondo, Hassan Hussen Yussuf, alisema hali inasikitisha katika harakati za kisiasa kuona Zanzibar inarejea katika siasa za chuki na uhasama.
“Matukio kama haya hutokea karibu na uchaguzi kwa kweli inasikitisha sana na kama halii itaendelea itakuwa hatari katika nchi,” Yussuf.
Alisema katika jengo hilo kulikuwa na
vifaa mbalimbali vya thamani na fedha taslimu za malipo ya uchukuaji wa
fomu za wagombea walizolipia zimeteketea.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani,
alisema CUF kinalihusisha tukio hilo kuwa ni joto la uchaguzi
na kuwashutumu waliofanya waliofanya tukio hilo kwani matukio kama hayo
yamekuwa yakifanywa inapokaribia kipindi cha uchaguzi mkuu.
“Hujuma
hizi zimepangwa na ni za makusudi kuchafua amani ya nchi,na hali kama
hii hutokea zaidi karibu na uchaguzi na CUF hufanyiwa hujuma mbalimbali
ikiwamo kuchomwa moto ofisi zetu,” Bimani.
-NIPASHE





Note: Only a member of this blog may post a comment.