Tuesday, March 31, 2015

Anonymous

NI BALAA! HII NDIO MITANDAO INAYOTEKETEZA ZAIDI WANAFUNZI NA VIJANA!

Tangu kuingia kwa miatandao ya kijamii nchini vijana wengi wamepata nafasi ya kuituma au kupokea ujumbe mfupi, picha na video; kwa njia rahisi zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Watumiaji wengi wa huduma hiyo hupendelea zaidi mitandao
inayowawezesha kutuma ujumbe wa siri kwa njia rahisi, mara nyingi watakavyo na kwa gharama ndogo. Kati yao, lipo kundi la wanafunzi linalopendelea kuwasiliana kwa njia ya kuandikiana ujumbe wa maandishi na kutumiana picha.

Kwa mujibu wa takwimu za Machi mwaka huu za Kampuni ya Utafiti ya Statista ya Marekani, mtandao wa Facebook ndiyo unaoongoza kwa kuwa na watumiaji wengi, ukifuatiwa na mtandao wa WhatsApp.

Mitandao mingine na idadi ya watumiaji wake kwenye mabano ni Qzone (watu milioni 629), Facebook Messenger (watu milioni 500), WeChat (watu milioni468), LinkedIn (watu milioni 347), na Twitter (watu milioni 288).
Pamoja na kuwa Facebook inatawala orodha ya watumiaji wa mitandao hiyo, wataalamu wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano wanasema kuwa miaka michache ijayo vijana wataanza kukimbilia mitandao mingine yenye ‘ladha’ tofauti.

Baadhi ya mitandao hiyo ni pamoja na Kik Messenger, ooVoo na WhatsApp inayowawezesha watumiaji wake kutuma ujumbe kwa urahisi. Kundi la vijana wanaopenda kutuma habari mbalimbali mitandaoni litalazimika kujikita kwenye mitandao ya Instagram, Tumblr, Twitter na Vine.

Kundi jingine ni la vijana wanaopenda kutuma ujumbe wa siri kwa rafiki au wapenzi wao. Kundi hili linavutiwa zaidi na mitandao ya Secret-Speak Freely, Snapchat, Whisper na Yik Yak.
Japokuwa uongozi wa Facebook umekuwa ukijaribu kuja na mbinu mpya kila siku ili kuendelea kuwashikilia wateja wake, bado msukumo wa kizazi kipya kujaribu mambo mapya unabaki kuwa uchaguzi pekee.

Kundi la mwisho ni la vijana wanaotumia muda wao mwingi kwa ajili ya kuchati na kupeana miadi mtandaoni. Kundi hili linavutiwa na mitandao ya MeetMe, Omegle, Skout na Tinder.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam Sunday Elisaria, anasema teknolojia ya mawasiliano ya simu imeleta matatizo kwa wanafunzi katika nchi za Afrika kuliko ilivyotarajiwa.

Elisaria anasema kama mwanafunzi angetumia simu kama chombo muhimu cha kumsaidia kupata taarifa za masomo, wasingelalamikia ukosefu wa vitabu uliopo katika shule na vyuo nchini.

“Sasa badala ya mwanafunzi kutumia mtandao wa ‘google’ kutafuta taarifa za kitaaluma, muda mwingi anachati na kutuma picha kwenye ‘Facebook’,” anasema Elisaria.

Kwa mujibu wa mtandao wa ‘Common Sense’, wazazi wanatakiwa kuelewa kuwa mtandao wa ‘Kik Messenger’ unaruhusu vijana kutuma ujumbe bure bila kikomo kwa haraka.

Watumiaji wa mtandao wa ‘ooVoo’ wanafurahia kuangalia picha za video bure, huku mtumiaji akiruhusiwa kuchati na watu hadi 12 bure.

Mtandao wa kijamii ambao pengine ndio ‘habari ya mjini’ hivi sasa wa ‘WhatsApp’, unamwezesha mtumiaji kutuma ujumbe, sauti, video na picha kwa mtu mmoja au wengi. Moja ya masharti ya ‘WhatsApp’ ni kuwa mtumiaji lazima awe na umri wa miaka zaidi ya 16.


Mwanafunzi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Edna John anasema wanafunzi wanaotumia ‘Facebook’ wameanza kuvutiwa na mtandao wa kijamii wa ‘Instagram’ kwa kuwa unamwezesha mtumiaji kupiga picha, kuzihariri na kuziweka mtandaoni. Pia unamwezesha mtumiaji kuweka video yenye sekunde 15.

‘Twitter’ inamwezesha mtumiaji kutuma ujumbe mfupi wa herufi 140. Mara nyingi hutumiwa na watu wazima ambao hupendelea kutuma ujumbe wa wazi, ingawa inawezekana pia kutuma ujumbe wa siri.

Mitandao hatari kwa vijana
Mitandao ya ‘Secret-Speak Freely’, ‘Snapchat’, ‘Whisper’ na ‘Yik Yak’, inatajwa kuwa ni hatari kwa vijana kwa sababu inawaruhusu kutumiana ujumbe wa siri au kutamka maneno yoyote wanayoyataka wakiwa na uhakika kuwa hakuna atakayewagundua.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.