Friday, February 27, 2015

Anonymous

MAKAVU LIVE: POLE DULLY ILA UMESAHAU HUO NDO’ UKUBWA?

NIMPE pole sana mdogo wangu Abdul Sykes kwa msiba mzito alioupata wiki mbili zilizopita, kwa kuondokewa na baba yake mzazi, mzee wetu Ebby Sykes. Ingawa kila mtu ana uchungu na kifo chake kinachomhusu, lakini kwa wengi wetu, kumpoteza baba au mama mzazi ni moja kati ya mapigo yanayotuumiza mno.

Mzee Sykes alifariki Februari 15, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu akiwa na umri wa miaka 62! 

Dully au kama mwenyewe anavyojikubali kuwa ni Mr Misifa, ni mmoja kati ya wasanii ambao wametoa mchango mkubwa katika muziki wa Bongo Fleva hadi kuufanya uwe kama hivi ulivyo leo.

Nimemfahamu tangu akiwa kijana mdogo kabisa, pale mitaa ya Kariakoo na nimeshuhudia akikua kiakili na kimuziki kiasi cha kumfanya hivi sasa kuwa mmoja wa mastaa wenye heshima na mafanikio ya kuelezeka. 

Ninamfahamu kama kijana mcheshi, mwenye utani mwingi kiasi kwamba siyo rahisi kumkuta Dully katika kundi akiwa msikilizaji. Nitakuwa namkosea heshima anayostahili kama nitajaribu kusema wimbo wake flani ndiyo unaomtambulisha. 

Alikwisha jitambulisha kitambo na ana nyimbo nyingi mno, lakini kwa uchache nikizitaja ni kama Salome, Nyambizi, Hi na Dhahabu. Muziki umempatia msanii huyu kumiliki studio mbili, ambazo zinatumika kurekodi kazi zake na hata za wenzake, bila kusahau kuwa vijana wengi wanaotamba sasa, wamepitia katika mikono yake. 

Lakini juu ya yote mazuri kwa Dully Sykes, kuna kauli moja aliyoitoa hivi karibuni kuhusu msiba wa baba yake, haikuwa ya kiungwana, kwa maoni yangu.Alinukuliwa akiviambia baadhi ya vyombo vya habari kuwa alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wasanii kutojitokeza kwenye msiba wa marehemu baba yake, kitendo alichodai kilimfanya ajisikie vibaya, kwani baadhi ya walioshindwa kwenda ni marafiki zake wa karibu, wengine wakimwita kaka! 

Tangu awali, nilisema ni kwa kiasi gani kumpoteza mzazi kunavyouma kwa sababu mara nyingi, wao ndiyo taa imulikayo maisha yetu. Lakini kuna jambo moja la msingi sana ambalo tunapaswa kulizingatia, hasa katika matukio kama haya. 

Misiba, tofauti na sherehe, ni vitu vya ghafla na visivyotarajiwa. Mtu anaweza kuwa katikati ya mishemishe ya kupata hela, tena kubwa, ghafla akapata taarifa za msiba wa baba au mama yake.

Kibinadamu, kama mishemishe hizo zinachukua zaidi ya siku moja, zinasimama na kinachopaswa mbele yake, ni kujishughulisha na msiba. 

Kwa sababu itashangaza sana kusikia mtu hayupo kwenye msiba wa mzazi wake, kisa kaenda mkoa kwenye mitikasi ya hela.Na tambua kitu kimoja, jinsi unavyoguswa na msiba wa mpendwa wako, sivyo itakavyokuwa kwa wanaokuzunguka, wawe marafiki, wafanyakazi wenzako au hata majirani. Unaweza kufiwa sasa hivi, na mshkaji wako akapata dili la hela akakuacha. 

Ni kujidanganya kudhani kwamba kutokana na ukubwa wa jina, utajiri au umaarufu, basi kila unayemfahamu atakuja msibani kwako.Kwa maana nyingine, kulalamika kwa f’lani kutokuja msibani kwako, ni kumvunja nguvu aliyefika, kwani inaonyesha kama yeye hakuwa na umuhimu. 

Wakati nikiamini kuwa ni jambo jema kuhudhuria misiba na matatizo ya jamaa, rafiki, jirani au mfanyakazi mwenzako, ni vyema pia kutambua kwamba mhusika mkuu wa matatizo yako ni wewe mwenyewe, wengine wanaokuja ni kuwashukuru.

Kulalamika kwamba flani hakuja wakati mtaani anakuita bro, mjomba au baba ni kumuonea kwa sababu hauna ratiba ya maisha yake. 

Mtu wako wa karibu anaweza kubanwa na mambo yake akashindwa kutokea msibani siku ya tukio, lakini kesho au keshokutwa atakuja na kukupa pole yake. Kulalamika kutomuona mtu msibani kunaweza kuwapa watu wengine tafsiri ya kwamba badala ya kuomboleza msiba, mtu alikuwa na kazi ya kuangalia nani na nani wamekuja au nani na nani walikuwa wanalia!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.