Friday, February 27, 2015

Anonymous

CHUJIO LA MGOMBEA PINDA ANAVYOFAA, ASIVYOFAA KUWA RAIS 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
HAKASIRIKI kuitwa mtoto wa mkulima maskini; huyu si mwingine ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyezaliwa Mpanda vijijini mkoani Katavi zamani ukijulikana kwa jina la Rukwa. Ni mtoto wa kwanza katika familia, mwenye Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyoipata mwaka 1974. 

Pinda amepata kuwa Wakili wa Wizara ya Katiba na Sheria, kazi aliyoanza kuifanya muda mfupi baada ya kuhitimu masomo yake chuoni.Mwaka 1978, kiongozi huyo alihamia ofisi ya usalama wa raia akifanya kazi chini ya awamu mbili  za marais Julius Nyerere na Ali Hassan Mwinyi. 

Kuanzia 1982, waziri mkuu huyo alipewa kazi ya kuwa Katibu Msaidizi wa Rais hadi 1992, ambapo baadaye alipangiwa kazi maalumu  ya kiusalama. Historia inaonesha kwamba, 1996 hadi 2000 aliteuliwa kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri kabla ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mpanda Mashariki katika uchaguzi wa 2000, ambapo alishinda kwa kishindo. 

Baada ya ushindi huo, Pinda aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Mwaka 2006, akapanda cheo na kuwa waziri kamili. Miaka miwili baadaye, kura 279 kati ya 283 zilimthibitisha kuwa mrithi wa kiti cha uwaziri mkuu, akiziba nafasi ya Edward Lowassa aliyejiuzulu kwa tuhuma za Richmond, nafasi ambayo amedumu nayo kwa miaka saba mpaka sasa. 

UTUMISHI WAKE
Pinda amekuwa ni kiongozi asiyekuwa na makeke, anayeishi maisha ya kawaida, msikivu na mwenye huruma. Amejipambanua mara kadhaa kuwa ni mwadilifu na mtu asiyejilimbikizia mali. 

Amewahi kutamka hadharani kwamba, akaunti yake ya benki ina kiasi cha shilingi milioni 20, jambo ambalo lilizua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii. “Miaka chungu nzima ya ajira serikalini, vipi awe na kiasi hicho cha fedha? Anaongopa!”  ndivyo zilivyokuwa hoja za wadadisi wa mambo ingawa hazikuweza kufuta kauli ya kiongozi huyo. 

Maisha ya utumishi serikalini yamempa mtaji mkubwa kuliko wagombea wengine. Pinda ni mtoto wa ikulu tangu zamani, siyo mgeni wa dhifa za wakubwa, amekula ujana wake akiwa karibu na viongozi wa nchi, kwa tafsiri za leo ananukia uaridi la ikulu akiwa na uzoefu wa kutosha alioupata kutoka kwa marais wa awamu zote nne. 

ANAFAA AU HAFAI KUWA RAIS?
Kwa kuwa mfumo wa sasa kikatiba unamtaka mgombea urais awe ni mwakilishi wa chama chake, ni vema kumchuja Pinda kwa kumwangalia kupitia sifa za mgombea zinazotakiwa na chama chake ambazo ni hizi zifuatazo: 

KWANZA: Awe na uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa kwa kuzingatia uzoefu wake katika uongozi wa shughuli za serikali, umma na taasisi. Kimtazamo, Pinda sifa hii anayo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya uongozi.
PILI:  Ni suala la elimu ya chuo jambo ambalo Pinda hana tatizo nalo.

TATU: Awe mwadilifu, asiyetiliwa shaka juu ya matendo yake ya uadilifu mbele ya uso wa jamii ya Watanzania na awe mwenye hekima na busara. Sifa hii pia anayo. 

NNE:  Awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha, kuimarisha na kuendeleza Muungano, umoja, amani, utulivu na mshikamo wa kitaifa. Hapa pana shida kidogo, kwani historia haimuoneshi waziri huyu kama ni mtu aliyewahi kuuhudumia muungano kwa namna yoyote, ingawa ni jambo ambalo siyo gumu kujifunza kwa kufuata miongozo ya nchi. Kwenye kudumisha amani anaweza kujipanga akiamua. 

TANO: Awe mtu mwepesi wa kuona mbali, asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu masuala nyeti na muhimu ya taifa kwa wakati unaofaa. Hiki kinaweza kuwa kikwazo kingine. Itakumbukwa kuwa Pinda alishindwa kuonesha kuona mbali kwake na kufanya uamuzi wa busara wakati wa sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, alipotuhumiwa kuandaa fedha za kuwahonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara yake. 

Kwenye sakata hili aliyumbishwa na mfumo kiasi cha kugwaya kumchukulia hatua kwa kisingizo kuwa alisubiri maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete.SITA: Awe na upeo mkubwa na usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi na dunia yote kwa ujumla. Kwa mtazamo wa kawaida, Pinda hana uzoefu wa masuala ya kimataifa, ingawa nafasi ya uwaziri mkuu imemsaidia kidogo kutambulika. 

SABA: Asiwe mtu mwenye hulka ya udikteta au ufashisti, bali awe anaheshimu na kulinda katiba ya nchi, sheria, utawala bora, kanuni na taratibu za nchi. Ingawa waziri huyu anatajwa kuwania nafasi ya urais, kipengele hiki kinamtoa kwenye sifa, kwa sababu mara kadhaa kwa kauli zake ameonesha kuwa yeye ni mwenye hulka ya udikteta mfano kauli yake ya: “Wapigwe tu” ambayo aliitoa kuonesha msisitizo wa kuwashughulikia wasiotii sheria. 

Aidha kauli ya wanaoua Albino nao wauawe aliyowahi kuitoa alipofanya ziara mikoa ya Kanda ya Ziwa inaashiria kuwa ni mtu mwepesi wa kukiuka katiba ya nchi inayoheshimu haki ya mtu kuishi. 

NANE: Awe mtetezi wa wanyonge, haki za binadamu, mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu wa mtu binafsi. Mpaka sasa Pinda hajaonesha nia yake ya kuwatetea wanyonge kwani mara kadhaa ameshindwa kukabiliana na rushwa, mdororo wa maisha ya wananchi na huduma duni za kijamii; ingawa si mtu wa kujitafutia umaarufu. 

TISA, Awe mstari wa mbele kuzifahamu, kuzitetea na kuzitekeleza sera za CCM na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Hapa tena panaweza pakawa na shida kidogo kwa kiongozi huyo kutokana na kuishi nje ya maisha ya siasa kwa muda mrefu. Pinda siyo zao la CCM kama alivyo Kikwete. 

KUMI:  Awe mpenda haki na mtu jasiri katika kupambana na dhuluma na maovu yote nchini. Kwa mtazamo, Pinda ameshindwa kuonesha ujasiri wa kupambana na maovu. Mwaka 2012 alinusurika kung’olewa kwa kura za kutokuwa na imani naye baada ya bunge kuwasulubu mawaziri wanane ambao walitajwa kuvurunda huku yeye akishutumiwa kwa kuonesha udhaifu wa usimamizi. 

Kama hilo halitoshi, Pinda huyuhuyu alishindwa kuonesha ujasiri wake kwenye sakata la Oparesheni Tokomeza ambalo baadhi ya mawaziri walifukuzwa na yeye kuponea chupuchupu kutimuliwa.
Aidha alivuna udhaifu kwa kushindwa kutambua wizi wa shilingi bilioni 300 kwenye akaunti ya Escrow na kibaya zaidi mwenyewe akituhumiwa kuhusika. 

KUMI NA MOJA: Asiwe mtu ambaye anatumia nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali. Jambo hili si kikwazo kwake. KUMI NA MBILI ambayo ni: Kwa ujumla awe ni mtu anayekubalika kwa wananchi. Hapa pana shida kubwa, tafiti nyingi ikiwemo ile iliyofanywa na taasisi ya TWAWEZA, Pinda haonekani kama ni mtu mwenye mtaji wa watu, hakubaliki sana miongoni mwa jamii. 

KUMI NA TATU: Awe mtu makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa viongozi/watendaji na asiyevumilia uzembe… Tofauti na mtangulizi wake Lowassa ambaye alionesha kukerwa na uzembe na uwajibikaji, Pinda amekuwa mkimya na asiyeonesha kukerwa na wazembe. 

Ni kiongozi ambaye anatajwa kuwa ni mpole au muoga kupita kiasi, jambo ambalo limetajwa kuwa sababu ya kuvurunda kwa watendaji wengi serikalini hasa katika kipindi cha uwaziri mkuu wake. Ni waziri mkuu ambaye huenda akaondoka bila kuonesha makucha ya kuwawajibisha wanaokwenda kinyume na matakwa ya nchi.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.