Wednesday, October 5, 2016

Unknown

Ni hatari kuiruhusu mitandao ya kijamii iwe kipimo cha upendo au chuki!

Niliipaki pikipiki yangu nje ya saluni ya Mwanaisha, maarufu mno maeneo yote ya Kitunda. Mwanaisha mwenyewe, licha ya kuwa shabaha ya kila mwanaume mwenyewe pesa maeneo yale, alikuwa msichana aliyejitunza, akatunzika, mgumu kumnasa. Alikuwa mwerevu, asiye na makuu.

Hicho kiliwakera wanaume wengi waliojiona si kitu kwake, hawakumbabaisha – kwa lipi kwanza? Kwasababu kama fedha alikuwa nazo. Wanasema alikuwa anaringa sababu mpenzi wake alikuwa mwanamuziki maarufu. Wanaume wa Kitunda aliwaona kama kama sazo la ngisi, na hawakuwa na vigezo vya kucheza ligi yake – wao ligi daraja la pili, yeye ligi ya ‘premier’ wangemweza vipi?

Saluni ilikuwa imechangamka kwa soga za marafiki waliokutana kijiweni kwao, hapo kwa Mwanaisha. Ni kama walikuwa hawajakutana kwa miaka mingi. Vicheko na sauti za viganja vilivyoganganishwa umbea uliponoga, viliyakaribisha masikio yangu.

Tangu jana, Mwanaisha alikuwa akinipigia simu nikamrekebishie swichi yake ya umeme aliyodai ilikuwa na mushkeli.

“Mimi nilijua tu yule anajishaua, hana lolote chuki zimemjaa, ndio maana sura imemkomaa kama jiwe la bafuni. Eti mzuri, ha ha ha, mzuri awe yule? Na Kim Kardashian tumwiteje?” Sauti ya Maimuna aliyekuwa kavalishwa mashini kubwa la saluni linalokausha nywele za akinadada wapendao kupendeza, ilisikika wakati nikifunua pazia kuingia ndani kuanza kazi – kazi niliyoitiwa na Mwanaisha.

“Hata siamini shoga, na kujipendeza kote kule, kumpa zawadi za kila aina, leo ndio anikaushe kama hanijui, kwenye siku yangu muhimu kama hii? Kweli imeniuma sana,” alisema Mwanaisha aliyekuwa amekaa kwenye kochi jeusi ndani ya saluni hiyo.

“Karibu Beka,” alinikaribisha kwa sauti ya unyonge. Nilionekana kuyakatisha mazungumzo yao yaliyokuwa yamekolea. “Asante Mrs Supastaa, swichi inayosumbua ndio ipi?” Nilimuuliza huku nikiyazungusha macho yangu kwenye chumba hicho kilichokuwa na fukuto la joto la Dar – joto kweli kweli!

“Ni hiyo hapo kwenye AC, hushangai joto la humu? Tumekuwa kama mikate kwenye oveni, linanipa hasira tu mimi na nshavurugwa hapa,” alisema Mwanaisha huku akijipuliza na kipande cha gazeti kulipunguza joto hilo. Michirizi ya kijasho chembemba ilionekana kushuka kwenye shingo yake nyeupe, nzuri na ndefu kama ya twiga.

“Poleni, naona tu mnavyotweta,” niliwapoza huku nikichukua begi langu kuchukua vifaa vya kazi.
“Wifi yako ana visa, gubu litamuua, uzuri wako unamtesa kama nini. Unavyohangaika kumposti kila siku, kumbe ulikuwa unajichora tu,” alisema mwanamke mwingine, mgeni machoni mwangu aliyekuwa amekaa kulia kwa Mwanaisha.

“Hata siku ile ameiweka ile picha mliyopiga mkiwa na G-Style, hakukumention, aliweka jina lako kavu kavu, kwani hajui handle yako?” Maimuna aliyekuwa bado kwenye mashini hilo kubwa akiunguzwa na mvuke wa moto alidakia.

Alipotaja jina la G-Style, masikio yangu yalipata hamu ya kusikia mkasa huo ulioonesha kuwatoa povu wanawake hawa wa Kitunda. G ndiye yule mpenzi wake na Mwanaisha, maarufu Dar nzima. Niliyatega masikio pima kujua lipi hilo la kuwajaza hasira walimbwende hawa.

“Anaijua sana, basi tu gubu lake, aliona labda angeniongezea followers,” alijibu Mwanaisha.
“Basi wewe siku yake ya birthday ukajiandikia posti ndefu kumsifia wifi yako, na siku ile ulipata comments nyingi kuliko siku zote,” alisema yule mwanamke mwingine huku kicheko kikimlipuka na kumwalika Maimuna uchekoni, aliunga tela. “Ha ha ha, haloo halooooooooooo, watu na mawifi zao wenye roho za kutu, mtakoma mwaka huu.”

Kicheko cha umbea kilitaka kumponza Maimuna. Almanusra adondoke kwenye kiti cha plastiki alichokuwa amekalia.“He shoga yangu, kaa vizuri usije ukaanguka nikakosa wa kupiga naye umbea miye,” alisema mwanamke yule kwenye kochi la Mwanaisha na kukaribisha vicheko vingine.

“Basi nikajua nimepata wifi, ukute hata hapendi niwe na kaka yake. Kila siku naona anavyowaposti mashoga zake, wifi ah ah!, hapostiwi, au mpaka nimuombe? Thubutu,” Mwanaisha aliyeonekana kuzidiwa na joto alisema kwa hasira.

Maongezi yao yalinipa picha kamili ya kile kilichokuwa kimeikera mioyo yao. Nilikuwa nimeshamaliza kurekebisha swichi na kiyoyozi kimeanza kupata uhai, joto linatafuta upenyo wa kukitoroka chumba kile.

Nilijaribu kujizuia kutoingilia maneno ya warembo hawa lakini nilishindwa. “Umekasirika wifi yako kutokuambiia happy birthday kwenye Instagram?” Maneno yalinichomoka mdomoni.
“Sana Beka,” Mwanaisha alijibu kwa pupa. “Kwani asipokuweka, wewe unapungukiwa nini?” Niliuliza nikisubiri jibu lake kwa shauku.

“Kama anampenda wifi yake ni lazima angemposti Instagram kumpongeza, huo ndio upendo wa kweli,” Maimuna alimjibia Mwanaisha. “Upendo wa kweli kumposti mtu Instagram?” Niliuliza.
“Ndio maana yake,” Mwanaisha na Maimuna waliitika kwa pamoja.

“Mwanaisha, umeifahamu lini Instagram? Ama basi umejiunga lini kwenye mtandao huo?” Nilimtupia swali jingine. Alijifikiria kwa muda. “Kama miaka miwili na nusu hivi.”

“Miaka miwili na nusu, mbona michache Mwanaisha? Kabla ya Instagram, ulikuwa unapima vipi upendo kwa mtu wako wa karibu?” Niliwauliza lakini swali lilionekana gumu na kuwapa ububu kwa muda.
“Hicho ndicho kinaharibu kizazi cha leo. Tunapima upendo kwa kuzingatia kile tunakiandika kwenye Instagram ama mitandao mingine ya kijamii. Tunapotea, tunakosea na hatupaswi kuendeleza imani hii,” nilihutubia na hadhira yangu iliendelea kunipa nafasi ya kuendelea.

“Instagram,WhatsApp, Facebook na hii nyingine inayowapa uchizi kabisa mastaa wetu sasa hivi, inaitwaje vile, jina limenitoka.. inaitwaa..”

“Snapchat,” alinisaidia Maimuna,

“Hewallaa, Snapchat. Hivi vimekuja juzi tu na vimetukuta na maisha yetu mengine kabisa. Mtu anapokuposti Instagram, Facebook au kwingine huko, haimaanishi kuwa anakupenda sana kuliko wengine. Na pia mtu asipofanya hivyo haimaanishi anakuchukia.”

“Ila kweli Mwanaisha, maneno ya Beka ya ukweli ndani yake,” mwanamke wa pembeni ya Mwanaisha aliniunga mkono.

Hasira za wanawake wale zilionekana kupungua kidogo. Sikujua ni kwasababu ya maneno yangu ama sababu kiyoyozi kilikuwa kimelitimua joto tayari. Sikutaka kuendelea na hotuba yangu kwakuwa wanawake wale walionesha kukinaishwa na hadithi ya wifi yao. Nilichukua begi langu kutaka kuianza safari nyingine baada ya kumaliza kilichokuwa kimenipeleka pale. Kabla sijaondoka, saluni ilipata ugeni wa ghafla. Alikuwa ni G-Style aliyeongezana na dada yake.

“Surpriseeee,” alisema Rukhsar, dada yake G-Style akiwa kajaa bashasha usoni. Kabla Mwanaisha hajasema lolote, Rukhsar na kaka yake walianza kumuimbia. “Happy birthday to you, happy birthday to you.”

Mwanaisha alikuwa bado amepigwa na butwaa. Wifi yake alichomoa boksi mpya ya simu ya iPhone 6 Plus na kumpa huku akimkumbatia. “Nakupenda sana wifi yangu,” alisema Rukhsar.

Nilijishtukia kwanini niliendelea kushangaa sinema ile. Nilijikumbusha kuwa muda wa mimi kuendelea kuwa pale ulikwishaisha zamani. Niliomba waniruhusu niwaache. Mwanaisha alinipa ujira wangu nikautia mfukoni, elfu 15 za chap chap. Nilitoka nje, nikawasha pikipiki yangu na kuondoka nikiwa na furaha kuwa nilichokihutubia muda mfupi uliopita kimepata ushahidi wenye nguvu.

-via bongo5

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.